Dec 30, 2019 02:42 UTC
  • Kuwait kuanzisha upya safari za ndege kwenda Yemen

Emad Al-Jalawi , Naibu wa Masuala ya Usalama na Amani ya Safari za Ndege na Uchukuzi nchini Kuwait amesema kuwa hivi karibuni safari za ndege kutoka nchi hiyo kwenda Yemen zitaanza.

Katika barua aliyomuandikia mkuu wa idara ya safari za ndege wa Yemen, ameridhia mpango huo wa kuanzishwa tena safari za ndege kati ya mataifa hayo mawili ya Kiarabu. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya makubaliano ya kiufundi ya lazima, inatazamiwa kuwa Kuwait itakuwa na safari tatu za ndege kwa wiki kutoka nchi hiyo kwenda Yemen na kinyume chake. Kuwait inakuwa nchi ya kwanza kati ya mataifa ya Ghuba ya Uajemi kuanzisha huduma zake za usafiri wa ndege nchini Yemen tangu muungano vamizi wa Saudia ulipoanzisha hujuma zake za kinyama ndani ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu mwezi Machi 2015. 

Emad Al-Jalawi, Naibu wa Masuala ya Usalama na Amani ya Safari za Ndege na Uchukuzi nchini Kuwait.

Katika hatua nyingine shakhsia na wanaharakati mbalimbali wa kisiasa na kijamii wa Kuwait wamelaani vikali hatua ya Spika wa Bunge la nchi hiyo ya kulikaribisha kundi moja la kigaidi linalopigania kujitenga na lililo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa mujibu wa wanaharakati na shakhsia hao, hatua ya Spika wa Bunge kulikaribisha kundi hilo la kigaidi ni kinyume na sheria na mikataba ya udiplomasia ambayo inatumika kati ya nchi za dunia na msingi wa ujirani mwema kama ambavyo ni uingiliaji wa masuala ya ndani ya Iran. Khalil Abdullah Abul, mmoja wa wabunge wa Kuwait ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter akikosoa jambo hilo na kulitaja kuwa 'Hatua hatari ya kisiasa.'

Tags