Dec 30, 2019 07:28 UTC
  • Wayamen karibu milioni 4 wamekuwa wakimbizi kutokana na mashambulio ya Saudia

Kituo cha Taarifa cha Baraza Kuu la Uongozi na Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu nchini Yemen kimetangaza kuwa, karibu watu milioni 4 wa nchi hiyo wamelazimika kuwa wakimbizi kufuatia mashambulio ya anga ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.

Ripoti iliyotolewa na kituo hicho inaeleza kuwa, raia milioni 3 na laki nane ya wa nchi hiyo wanaishi katika hali mbaya kutokana na kutokuwa na makazi na hivyo kulazimika kutangatanga huku na kule.

Ripoti hiyo imeashiria hali mbaya wanayokabiliwa nayo wakimbizi hao na kusema kuwa, idadi ya familia zinazoishi katika maisha ya ukimbizi na kutokuwa na makazi iliongezeka katika mwezi uliopita wa Novemba.

Kituo cha Taarifa cha Baraza Kuu la Uongozi na Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu nchini Yemen kimekosoa kile kilichokitaja kuwa 'uzembe' wa taasisi za kimataifa katika kuwasaidia raia hao.

Yemen inavyoendelea kubomolewa kufuatia mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake

Takriban miaka mitano imepita sasa tangu Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu  (Imarati) zianzishe mashambulizi ya kila upande dhidi ya nchi maskini ya Kiislamu na Kiarabu ya Yemen. Zaidi ya watu 16 elfu wameshauawa, makumi ya maelfu wameshajeruhiwa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi kutoka na ukatili unaofanywa na wavamizi hao wa Yemen.

Uvamizi huo dhidi ya nchi maskini ya Yemen umewasababishia wananchi matatizo mengine mengi kama vile upungufu mkubwa wa chakula na madawa huku asasi mbalimbali zikiendelea kutahadharisha kwamba, hali ya kibinadamu ya nchi hiyo inazidi kuzorota siku baada ya siku.

Tags