Jan 16, 2020 07:42 UTC
  • Uturuki na undumakuwili wa kijeshi na kidiplomasia kuhusu masuala ya Asia Magharibi

Katika hali ambayo viongozi wa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki wameamua kutumia wenzo wa kijeshi kutatua matatizo ya Wakurdi wa nchi hiyo, wakati huo huo wanasisitiza kuwa matatizo ya pande zinazozozana katika eneo yanapasa kupatiwa ufubuzi kwa njia ya kisiasa na ya amani.

Kuhusiana na  suala hilo, Hulusi Akar Waziri wa Ulinzi wa Uturuki amesisitiza  kupatiwa ufumbuzi matatizo ya eneo kwa kustafidi na wenzo wa kisiasa. 

Hulusi Akar amesema: Ankara inatekeleza shughuli mbalimbali katika taasisi za kimataifa kwa lengo la kulinda maslahi ya Uturuki. Ni wazi kuwa serikali ya Ankara inafanya juhudi za kurejesha amani na uthabiti huko Libya na Syria na pia kusitisha umwagaji damu na kurejesha maisha ya raia wa nchi hiyo katika hali ya kawaida. 

Matamshi hayo ya Waziri wa Ulinzi wa Uturuki yametokana na kuchukuliwa misimamo ya kindumakuwili ya viongozi wa serikali ya Erdogan kuhusu masuala ya eneo. 

Hulusi Ankar amezungumzia wenzo wa kisiasa kuhusu amani na kurejesha hali ya uthabiti katika eneo katika hali ambayo serikali ya Uturuki kivitendo imechangia kumtwisha jirani yake hali ya vita isiyo na uwiano kutokana na hatua yake ya kukalia kwa mabavu sehemu za ardhi ya Syria. Wakati huo huo mbali na wananchi na vyama vya kisiasa; serikali huru za eneo zimewasisitizia mara kadhaa viongozi wa Ankara kuhusu suala la kufanya mazungumzo na Wakurdi wa Uturuki ili kufikia amani. Hata hivyo serikali ya Bwana Erdogan imepuuza njia ya mazungumzo na  kuendelea kupiga ngoma ya vita dhidi ya Wakurdi wa nchi hiyuo na wale wa Syria na Iraq. 

Rais Erdogan wa Uturuki 

Kwa hakika tunapasa kusema kuwa katika hali ambayo Waziri wa Ulinzi wa Uturuki anasisitiza kutumika njia ya mazungumzo kati ya pande zinazozozana katika eneo kwa lengo la kutatua matatizo na hitilafu mbalimbali kati ya pande hizo, kivitendo nchi hiyo siku zote inatumia njia ya kijeshi kutatua hitilafu zake na Wakurdi wa Uturuki na wa nchi nyingine jirani. Kuhusiana na suala hilo inaonekana kuwa viongozi wa Uturuki wamekusudia kuziweka katika ajenda yao ya kazi siasa hizo za kijeshi mkabala na kadhia ya Libya pia.  

Wapiganaji wa Kikurdi wa Uturuki 

Uturuki imeikalia kwa mabavu ardhi ya Syria katika hali ambayo nchi hiyo haikuwa katika hali munasibu sana kutokana na uwepo wa makundi na mirengo ya kitakfiri na kigaidi inayoungwa mkono na baadhi ya serikali za Magharibi na pia uingiliaji kati na njama za Marekani na baadhi ya serikali za Kiarabu za pambizoni mwa Ghuba ya Uajemi.

Kwa ibara nyingine ni kuwa katika pale ambapo Syria haikuwa na uwezo kamili wa kulinda ardhi yake; serikali ya Uturuki imetumia vibaya hali hiyo na kutuma wanajeshi wake nchini humo. Aidha serikali ya Uturuki imedhihirisha wazi msimamo wake ili kutimiza malengo yake huko Syria. Kuhusiana na suala hilo Matin Gurchan mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mwandishi mtajika wa Kituruki anaashiria hali mahsusi ya serikali ya Erdogan na kukaribia kuchukua maamuzi muhimu na kusema: Uamuzi muhimu wa Ankara ni kuchagua baina ya Marekani au muungano wa Russia-Iran. Ankara hadi sasa ilikuwa imefanikiwa kufuatilia stratejia mbili zinazoendana huko Syria na Iraq; na kunufaika kikamilifu na vita vya kuwania madaraka kati ya pande hizo. Hata hivyo stratejia hiyo sasa imefikia mwisho. 

Mchambuzi huyo wa Kituruki ameashiria ukweli huu wa mambo kwamba zile zama za Uturuki kujidhihirisha  kuwa huru kuhusu masuala mbalimbali ya eneo khususan huko Syria na Iraq zimefikia tamati. Wakati huo huo kuhusu uingiliaji wa kijeshi wa Uturuki katika masuala ya nchi nyingine za eneo ukweli huu wa mambo pia haupasi kupuuzwa kwamba uingiliaji huo wa nje ya mipaka ya nchi haupo katika uwezo wa wanajeshi wa Uturuki. Ni wazi kuwa uwezo wa kiuchumi wa Uturuki hautoi fursa ya kuendelea kwa muda mrefu mchakato huo wa uingiliaji mambo ya nchi nyingine. Aidha kuendelea mchakato huo huenda kukawa tishio kwa nguvu ya kitaifa ya Uturuki.  

Maoni