Jan 16, 2020 07:57 UTC
  • Israel kuendelea kujenga vitongoji vya walowezi licha ya malalamiko ya walimwengu

Utawala haramu wa Israel umetangaza kuwa, utaendelea na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Palestina unayoyakalia kwa mabavu.

Hayo yameelezwa na Eli Cohen, Waziri wa Uchumi wa utawala huo ghasibu alipotembelea kitongoji cha walowezi cha Beit El ambapo amesisitiza kuwa, utawala huo utaendelea na ujenzi na upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi.

Wakati huo huo, Naftali Bennett, Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel ametangaza kuwa, utawala huo una mpango wa kuanzisha maeneo saba yenye hifadhi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kupanua maeneo mengine 12.

Naftali Bennett, Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel

Disemba mwaka uliopita, Nikolai Miladinov , mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati alisema kuwa, mwenendo wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika eneo la Ukingo wa Magharibi na Quds Mashariki huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu uliongezeka kwa asilimia 70 mwaka huo ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.

Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu umeshika kasi zaidi tangu Rais Donald Trump aliposhika hatamu za kuongoza Marekani.   

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hadi sasa hakujachukuliwa hatua yoyote ya kutekeleza azimio nambari 2234 la tarehe 23 Disemba 2016 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. 

Tags

Maoni