Jan 17, 2020 02:52 UTC
  • Kamati ya usalama Iraq: Marekani haijawa na nafasi yoyote ya kuimarisha usalama nchini

Mjumbe mwandamizi wa kamati ya usalama na ulinzi ya bunge la Iraq amesema kuwa askari vamizi wa Marekani hawajawahi kuwa na nafasi yoyote ya kuimarisha usalama na amani nchini humo.

Ali Al-Ghanemi aliyasema hayo Alkhamisi ya jana ambapo sambamba na kusisitizia kutokuwepo makubaliano yoyote yanayohalalisha uwepo wa askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq amesema kuwa, huko nyuma karibu askari laki mbili na elfu 50 wa Kimarekani walikuwepo Iraq ambapo kutokana na makubaliano ya kistratijia kati ya Baghdad na Washington, hatimaye askari hao vamizi walilazimika kuondoka nchini humo. Ali Al-Ghanemi amebainisha kwamba kwa msaada wa maafisa usalama na wanachama wa Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi, Iraq iliweza kulishinda kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) sambamba na kuvuka mazingira magumu, lakini pamoja na hayo baadhi ya mirengo ya kisiasa na wafuasi wao wamekuwa na misimamo ya kindumakuwili kuhusiana na suala la ulazima wa kuodoka askari wa Marekani ambao hawajawahi kuwa na nafasi yoyote ya maana katika kuimarisha usalama na amani nchini Iraq.

Bunge la Iraq

Hayo yanajiri katika hali ambayo katika siku za hivi karibuni Adil Abdul-Mahdi, Waziri Mkuu wa Iraq amekuwa akifanya mazungumzo magumu na viongozi wa kieneo na wa madola ya Magharibi kuhusu kuondoka askari wa Kimarekani nchini humo. Kufuatia kitendo cha kinyama cha Marekani cha kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq, wabunge wa nchi hiyo walipitisha mswada wa kuwatimua askari vamizi wa Kimarekani kutoka ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Tags

Maoni