Jan 17, 2020 08:03 UTC
  • Ujumbe wa mwito wa maandamano ya milioni ya watu wa kuipinga Marekani nchini Iraq

Mwito uliotolewa na Muqtada al Sadr, mkuu wa mrengo wa Sadr nchini Iraq wa kufanyika maandamano ya milioni ya watu kuitaka Marekani iondoke nchini humo umepokewa kwa furaha na makundi ya muqawama na wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Siku ya Jumanne ya tarehe 14 Januari, Muqtada al Sadr aliwataka wananchi wa Iraq kuitumia leo Ijumaa kufanya maandamano makubwa ya milioni ya watu kulaani kuweko wanajeshi vamizi wa Marekani nchini humo. Mwito huo umepokewa haraka na makundi ya muqawama na wananchi wengi wa Iraq. Hatua hiyo imetoa ujumbe maalumu kwa walimwengu.

Ujumbe wa kwanza wa hatua ya makundi ya muqawama ya Iraq kuitikia haraka mwito huo wa kufukuzwa wanajeshi wa Marekani nchini humo, ni kwamba makundi hayo yote yanakubaliana kwa kauli moja na suala hilo. Kabla ya hapo Marekani ilifanya njama nyingi za kujaribu kuonesha kuwa kuna mizozo na mivutano baina ya makundi ya Kishia, lakini baada ya viongozi wa Washington kufanya jinai ya kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha al Hashd al Shaabi na watu wengine wanane waliokuwa wamefuatana nao karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad, makundi ya muqawama ya Iraq yamethibitisha kivitendo kuwa yana kauli moja kuhusu ugaidi wa wanajeshi wa Marekani. Mhimili mkuu wa kauli hiyo moja ya makundi ya muqawama ya Iraq, ni kufukuzwa wanajeshi wote wa Marekani nchini humo.

Hadi al Amiri  Mkuu wa Muungano wa Fat'h nchini Iraq

 

Kauli hiyo moja ya makundi ya Iraq ina na ujumbe mwingine nao ni kwamba stratijia ya Donald Trump wa kuwaua kigaidi makanda wa muqawama na kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya al Hashd al Shaabi ni stratijia ghalati na mbovu iliyotokana na kukosea mahesabu na matokeo yake imekuwa na madhara makubwa kwa Marekani na itaendelea kuwa na madhara makubwa kwa dola hilo la kibeberu.

Talib al Hasani, mchambuzi wa gazeti la al Rai al Yaum ameandika: Mwito wa maandamano ya milioni ya watu ya kushinikiza wanajeshi wa Marekani wafukuzwe nchini Iraq, umeisukuma Washington kwenye mkwamo mkubwa na kwamba juhudi za serikali ya Trump za kutumia makundi yake ndani ya Iraq haziwezi kusaidia kitu kwani idadi ya wafuasi wa Marekani ni ndogo nchini humo.

Ujumbe wa tatu muhimu wa mwito wa maandamano ya milioni ya watu ya kuipinga Marekani nchini Iraq ni kwamba makundi ya nchi hiyo hususan ya Kishia yanapinga vikali udhibiti wa aina yoyote ile wa Marekani katika masuala ya Iraq. Makundi hayo muda wote yanahimiza na kupigania kivitendo uhuru wa kujitawala taifa lao. Wakati akiitisha maandamano hayo ya milioni ya watu, Muqtada al Sadr alisema, nina yakini kwamba taifa la Iraq litawathibitishia wote kuwa, haliko tayari kujidhalilisha mbele ya ubeberu wowote bali Mwenyezi Mungu tu Ndiye Pekee wa kumnyenyekea si kiumbe chochote.

Bunge la Iraq limepasisha kufukuzwa wanajeshi wote wa Marekani nchini humo

 

Ujumbe wa nne ni kwamba makundi ya Kishia yana taathira kubwa katika siasa za Iraq, katika kupambana na adui wa nje na katika kulinda maslahi ya taifa la Iraq. Ni kwa sababu hiyo ndio maana kabla ya kutolewa mwito wa kufanyika maandamano hayo, kulifanyika kikao baina ya Muqtada al Sadr na viongozi wa makundi kadhaa ya muqawama akiwemo Hadi al Amiri  Mkuu wa Muungano wa Fat'h. Jambo hilo limeleta matumaini makubwa ya kupatiwa ufumbuzi wa haraka mgogoro wa kisiasa wa Iraq na kuelekezwa nguvu kwenye mapambano dhidi ya Marekani. Lakini pia uwezekano wa Marekani kutumia makundi yake kuanzisha wimbi jipya la maandamano nchini Iraq nao upo.

 

Maoni