Jan 18, 2020 03:10 UTC
  • Wajordan waandamana kupinga makubaliano ya gesi na Israel

Mamia ya wananchi wa Jordan wamefanya maandamano ya kupinga hatua ya serikali ya nchi hiyo kufikia mapatano ya mabilioni ya dola ya gesi asilia na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Maandamano hayo yaliyoratibiwa na asasi za kiraia zikiongozwa na 'National Campaign Against the Gas Agreement with the Zionist Entity' yalifanyika jana baada ya Sala ya Ijumaa katika barabara za mji mkuu Amman.

Waandamanaji hao wameitaka serikali ya nchi hiyo inayoongozwa  na Waziri Mkuu, Omar Razzaz ijiuzulu mara moja kwa kufunga mkataba wa ununuzi wa gesi na utawala huo haramu.

Kadhalika wamelitaka Bunge ambalo kesho Jumapili litakuwa na kikao lipige kura ya kuvunja makubaliano hayo ya Amman kuagiza gesi asilia kutoka Tel Aviv yenye thamani ya dola bilioni 10.

Wajordan katika maandamano ya kutaka kufungwa ubalozi wa Israel nchini humo

Aidha wananchi hao wa Jordan wametoa mwito wa kukamatwa na kufunguliwa mashitaka ya jinai maafisa wote waliohusika kufunga mkataba huo wa gesi asilia na utawala pandakizi wa Israel ambao ni wa miaka 15.

Maandamano kama haya yalishuhudiwa wiki iliyopita katika mji wa Zarqa ulioko kaskazini mashariki mwa Jordan, ambapo Meya wa mji huo Imad al-Momani aliyeshiriki maandamano hayo, aliitaka serikali ya Amman kufuta mara moja makubaliano hayo na Tel Aviv, aliyoyataja kuwa fedheha.

Tags

Maoni