Jan 18, 2020 07:31 UTC
  • Saudia yaipa Washington dola milioni 500 kwa ajili ya uwepo wa askari wa US nchini humo

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imefichua kuwa, utawala wa Riyadh umeipa Washingon dola milioni 500, kama malipo ya kugharamia uwepo wa askari wa Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Msemaji wa Pentagon, Rebecca Rebarich amesema mwezi uliopita wa Disemaba 2019, Riyadh iliipa Washington mamilioni ya dola za kugharamia operesheni za kijeshi za Marekani nchini humo.

Amesema, "Ili kwenda sambamba na muongozo wa Rais wa kuongeza gharama za kubeba mzigo pamoja na washirika wetu, Wizara ya Ulinzi ya Marekani imezungumza na Saudi Arabia kuhusu kubebea pamoja mzigo wa kuwepo askari wetu nchini humo kwa ajili ya kuimarisha usalama wa eneo na kuzima uvamizi. Riyadh imekubaliana na ombi hili na tayari imetoa mchango wake katika hatua ya kwanza."

Wiki iliyopita, Rais Donald Trump alidai kuwa tayari Saudia imeipa Marekani dola bilioni moja kwa ajili ya kugharamia uwepo wa askari wa Kimarekani katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Trump na Mfalme wa Saudia wakisaini mauzo ya silaha ya dola bilioni 110 mjini Riyadh

Akizungumza katika mkutano wa kampeni, Trump alisema, "tunatuma askari zaidi nchini Saudi Arabia na Saudia inatulipa kwa ajili hiyo. Niliwaambia nyinyi ni nchi tajiri, je, mnataka askari zaidi? Nitakutumieni askari zaidi lakini lazima mgharamie, na wanagharamia, tayari wameshatia dola bilioni moja kwenye akaunti yetu ya benki."

Juni mwaka uliopita 2019, miezi michache baada ya kuwafananisha viongozi wa Saudia na ng'ombe mkamwa maziwa, Trump alitoa matamshi mengine ya kudhalilisha dhidi ya watawala wa Aal-Saud akisema kuwa, kilicho muhimu kwake ni pesa za viongozi hao si kitu kingine.

Tags

Maoni