Jan 18, 2020 14:07 UTC
  • Mufti 'tipwatipwa' wa DAESH mwenye uzito wa kilo 245 atiwa nguvuni mjini Mosul, Iraq

Vikosi vya usalama vya Iraq vimemtia nguvuni Abu Abdul Bari, mufti wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) katika mji wa Mosul, kaskazini mwa nchi hiyo. Abu Abdul Bari ni maarufu kwa utoaji fatua za kuwafanya wanawake watumwa, za ubakaji, utesaji na uangamizaji wa kimbari.

Taarifa iliyotolewa na maafisa wa usalama wa Iraq imeeleza kuwa, mufti huyo wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) anayejulikana pia kwa jina la Shifa al-Nima alihamishwa kutoka mafichoni alikokuwa na kupelekwa kizuzini kwa kutumia gari la aina ya pikapu baada ya kushindikana kumchukua kwa kutumia gari ya polisi kutokana na uzito wake.

Bari ni maarufu pia kwa utoaji hotuba za kichochezi dhidi ya vikosi vya usalama vya Iraq na anajulikana kama mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa kundi la ukufurishaji la Daesh.

Aliwahi kutoa fatua ya kuamuru kuuawa mashekhe na maulamaa waliokataa kutoa kiapo cha utiifu kwa Daesh, wakati kundi hilo la kigaidi lilipovamia na kuukalia kwa mabavu mji wa Mosul mwaka 2014.

Magaidi wa kundi la ukufurishaji la DAESH (ISIS)

Mufti huyo wa Daesh alitoa amri pia ya kubomolewa turathi za kiutamaduni za mji huo hususan msikiti wa Nabii Yunus, hatua ambayo iliamsha hasira na kulaaniwa katika ulimwengu wa Kiislamu.

Itakumbukwa kuwa, aliyekuwa waziri mkuu wa Iraq Haidar al-Abadi alitangaza tarehe 9 Desemba 2017 kuwa siku ya kukamilika operesheni ya kuliangamiza kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Tarehe 10 Julai mwaka huo, Al-Abadi alitangaza ushindi dhidi ya kundi hilo katika mji wa Mosul uliokuwa ngome yake kuu.../

Tags

Maoni