Jan 19, 2020 02:54 UTC
  • Kuongezeka ukosefu wa usalama wa chakula Ukanda wa Ghaza

Tarehe 29 mwezi Dei sawa na Tarehe 19 Januari katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepewa jina la 'Siku ya Ghaza'. Katika kukaribia siku hii, Kamati ya Wananchi ya Kupambana na Mzingiro wa Ghaza imesisitiza kuwa ukosefu wa usalama wa chakula miongoni mwa wakazi wa Ukanda wa Ghaza mwaka jana wa 2019 ulifikia asilimia 70.

Ukosefu wa usalama wa chakula huko Ghaza unasababishwa hatua za utawala wa Kizayuni, Marekani na Mamlaka ya Ndani ya Palestina na vilevile kupuuzwa kadhia ya Palestina katika siasa za kimataifa. Utawala wa Kizayuni umeuzingira kwa pande zote Ukanda wa Ghaza tangu mwaka 2006 hadi sasa yaani kwa muda wa karibu miaka 14. Hali hiyo ya mambo imeathiri vibaya uchumi wa Ukanda wa Ghaza; kiasi kwamba wastani wa mapato ya kila siku ya mkazi wa eneo hilo ni karibu dola mbili huku kiwango cha Wapalestina wasio na ajira pia kikiwa zaidi ya asilimia 60. Wakati huo huo utawala wa Kizayuni kila mwaka unazuia kutumwa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo ile ya chakula huko Ghaza. Uhaba mkubwa wa chakula ni moja ya taathira za wazi za hali hiyo ya mambo. Kuhusiana na suala hilo, Jamal al Khudhr Mkuu wa Kamati ya Wananchi ya Kukabiliana na Mzingiro wa Ghaza amesema kuwa kuendelea kuzingirwa eneo la Ukanda wa Ghaza kumeifanya hali ya kiuchumi kuwa mbaya sana; jambo ambalo limesababisha pia ukosefu wa usalama wa chakula katika eneo hilo. 

Wanaharakati wa Palestina katika maandamano ya kutaka kuondolewa mzingiro wa Ghaza  

Aidha hatua zinazotekelezwa na Marekani ni moja ya sababu za kushuhudiwa ukosefu wa usalama wa chakula katika Ukanda wa Ghaza. Marekani mwaka juzi wa 2018 ilisitisha msaada wa dola milioni 360 kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA). Washington ilisema kuwa ilichukua hatua hiyo ili kuyashinikiza makundi ya KIpalestina yakubali mpango wake wa kibaguzi kwa jina la "Muamala wa Karne." Hata hivyo hatua hiyo imeshadidisha matatizo ya wananchi na maafa ya kibinadamu huko Ghaza.  

Aidha hatua zinazotekelezwa na Mamlaka ya Ndani ya Palestina pia zimekuwa na nafasi kuu katika kujitokeza hali hiyo ya ukosefu wa usalama wa chakula katika Ukanda wa Ghaza. Mamlaka ya Ndani ya Palestina kivitendo haitilii maanani wala kushughulikia matatizo na changamoto za raia wa Ghaza kwa kuzingatia hitilafu za kisiasa ambazo imekuwa nazo na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na Jihadul Islami. Ni miezi kadhaa sasa ambapo wafanyakazi wa Ukanda wa Ghaza hawajalipwa mishahara yao. Mamlaka ya Ndani ya Palestina inawashinikiza raia wa Kipalestina wa eneo hilo ili wakabaliane na makundi ya muqawama na hivyo kuipa mamlaka hiyo mwanya wa kutimiza malengo yake ya kisiasa katika eneo hilo. Natija ya hatua zote hizo na kuibuliwa undumakuwili huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza kumeshadidisha matatizo na masaibu ya wananchi wa Ghaza kukiwemo kuongezeka pakubwa ukosefu wa usalama wa chakula. 

Ukosefu wa usalama w chakula Ukanda wa Ghaza

Nukta muhimu hapa ni hii kuwa si tu kuwa licha ya kupita muda matatizo ya wananchi wa Ghaza hayajapungua bali yameongezeka zaidi. Ripoti mbalimbali za Ofisi ya Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika Ardhi za Palestina Zinazokaliwa kwa Mabavu zinaonyesha kuwa mwaka juzi wa 2018 karibu asilimia 65 ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza walikabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula; na kiwango hicho kilifikia zaidi ya asilimia 70 mwaka jana wa 2019. Kadhia hii kuliko mambo mengine, inaashiria na kudhihirisha waziwazi kwamba kadhia ya Palestina imepuuzwa katika siasa za kimataifa; na hata katika ulimwengu wa Kiarabu kadhia hiyo imefanywa tu kuwa suala la lenye umuhimu wa daraja la pili. Masuala mengine kama matukio ya ndani ya Iraq, vita vya Yemen na kuongezeka mivutano katika eneo la Asia Magharibi yana umuhimu mkubwa kutokana na taathira  ya nafasi ya madola ya kieneo na ajinabi katika eneo hili. Hali hii pia ni sababu muhimu ya kuongezeka matatizo huko Ukanda wa Ghaza khususan hali ya ukosefu wa usalama wa chakula unaoshuhudiwa sasa. 

Maoni