Feb 15, 2020 13:52 UTC
  • Viongozi wa Uturuki waendelea kutoa kauli za vitisho dhidi ya Syria kuhusiana na Idlib

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ametoa indhari ya kitakachotokea endapo mazungumzo ya nchi hiyo na Russia kuhusu kadhia ya Idlib hayatokuwa na tija.

Mevlüt Çavuşoğlu ametoa indhari hiyo leo na kueleza kwamba: Ujumbe wa Uturuki siku ya Jumatatu tarehe 17 Februari utaelekea Moscow kwa mazungumzo na viongozi wa Russia kuhusu Idlib, lakini kama mazungumzo hayo hayatokuwa na tija, Ankara itachukua hatua nyingine kuhusiana na suala hilo.

Duru ya pili ya mazungumzo baina ya jumbe za Uturuki na Russia ya kutafuta njia ya ufumbuzi wa kisiasa kwa lengo la kuhitimisha mgogoro wa eneo la Idlib la kaskazini mwa Syria ilifanyika siku chache zilizopita mjini Ankara, Uturuki, lakini ilimalizika bila kufikiwa mwafaka.

Sambamba na matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, shirika la haki za binadamu la Syria lenye mfungamano na makundi ya upinzani limetangaza kuwa, msafara uliobeba zana za kijeshi wa jeshi la Uturuki leo umeingia katika mikoa ya Idlib na Aleppo nchini Syria.

Askari na vifaru vya jeshi la Uturuki ndani ya ardhi ya Syria

Msafara huo mpya wa zana za kijeshi wa jeshi la Uturuki umeingia katika miji hiyo ya ardhi ya Syria, wakati jeshi la nchi hiyo linaendelea kusonga mbele katika mikoa hiyo miwili na kuyatimua makundi ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo.

Kwa muda wa karibu miezi miwili sasa, jeshi la Syria limeanzisha operesheni ya kuwatimua na kuwatokomeza magaidi katika mkoa wa Idlib; na hadi sasa limepiga hatua kubwa katika operesheni hizo, hata hivyo Uturuki inapinga operesheni hizo na imeamua kuvamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Syria kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.../ 

 

Tags

Maoni