Feb 16, 2020 11:00 UTC
  • Saudia imeshindwa katika vita dhidi ya Yemen

Kuvunjika makubaliano ya Riyadh, kuondoka kikamilifu askari wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kutoka Yemen na kutunguliwa ndege ya kivita aina ya Tornado ya muungano vamizi wa Saudia, kabla ya jambo lolote lile, ni mambo yanayoashiria kushindwa serikali ya Riyadh katika vita vyake vya kichokozi dhidi ya Yemen.

Vita vya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Yemen vilianza tarehe 26 Machi 2015. Hivi sasa vita hivyo vinakaribia kuingia mwaka wake wa sita, hata hivyo si tu kwamba vinaonyesha kutokuwepo ushindi wowote kwa Saudia, bali vinaonyesha kushindwa wazi utawala huo wa Aal Saud. Katika uwanja huo Jumatatu iliyopita Rajih Badi, Msemaji wa Serikali iliyojiuzulu ya Yemen alielezea kufeli mapatano ya Riyadh ambayo yalifikiwa Novemba mwaka jana chini ya upatanishi wa Saudia kati ya Baraza la Mpito la Kusini na serikali iliyojiuzulu ya Yemen kwa lengo la kuhitimisha mapigano nchini humo. Kuvunjika kwa mapatano ya Riyadh kuna maana ya kufeli juhudi za kisiasa za Saudi Arabia kwa ajili ya kuyaunganisha makundi ya Yemen, hususan ya kusini mwa nchi hiyo. Aidha Jumanne iliyopita Issa Mazroui, Kamanda wa Operesheni za Pamoja za Imarati nchini Yemen alielezea habari ya kuondoka kikamilifu askari wa nchi yake huko Yemen. Kuondoka kikamilifu askari wa Imarati nchini Yemen kumepelekea kusambaratika operesheni za muungano vamizi wa Saudia ambapo sasa Riyadh italazimika kuendeleza vita hivyo peke yake. Naye Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen pia Jumamosi asubuhi alitangaza kuwa ndege ya kivita aina ya Tornado ya muungano vamizi wa Saudia ilitunguliwa wakati ikitekeleza operesheni zake za kiuhasama katika mkoa wa Al Jowf. Kwa mujibu wa Kamanda Saree, ndege hiyo ilitunguliwa kwa makombora ya kisasa ya nchi kavu kwa anga yaliyozatitiwa kwa teknolojia ya kisasa.

Muqawama wa Jeshi na Harakati ya Answarullah ya Yemen umefelisha njama za Saudia, Marekani na marafiki wao

Ndege ya kivita aina ya Tornado ni ndege iliyoundwa kwa ushirika wa nchi za Uingereza, Ujerumani na Italia. Aidha kutunguliwa ndege hiyo mbali na kwamba kunakamilisha kushindwa kwa wiki za hivi karibuni kwa Saudia katika vita vyake nchini Yemen, pia kuna nukta nyingine kadhaa za kuzingatiwa. Mosi ni kwamba pamoja na uwepo wa mzingiro wa kila upande dhidi ya Yemen unaofanywa na utawala wa Aal Saud, lakini uwezo wa kiulinzi wa jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu, umefikia kiwango ambacho mbali na kusambaratisha ndege zisizo na rubani, pia unaweza kuangamiza hata ndege za kisasa za muungano vamizi wa Saudia. Katika uwanja huo pia, Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen, amesisitiza kuwa kuangamizwa kwa ndege hiyo ya kivita kunaonyesha kuwa anga ya Yemen sio eneo la kujifaragua tena maadui na badala yake maadui hao wanatakiwa kwanza kufanya mahesabu mara 1000 kabla ya kutekeleza hujuma zao. Pili ni kwamba sambamba na kukaribia kumalizika mwaka wa tano wa vita hivyo, Saudi Arabia imekumbwa na hali ya mtikisiko mkubwa. Kabla ya hapo majeshi ya Yemen yalitekeleza operesheni iliyopewa jina la Bunyaanul-Marsus katika eneo la kilomita mraba 2500 katika mikoa ya Nahum, Marib na Al Jowf. Kutunguliwa ndege ya Tornado kumeonyesha kwamba majeshi ya Yemen mbali na kuwa na uwezo wa nchi kavu, pia limejiimarisha katika uga wa anga kwa ajili ya kutoa pigo kali dhidi ya Saudia.

Baada ya ndege ya kisasa ya Saudia aina ya Tornado kutunguliwa nchini Yemen

Mafanikio hayo ya kijeshi ambayo yameenda sambamba na kushindwa kisiasa kwa utawala wa Aal-Saud, kumeikasirisha mno Saudi Arabia na hivyo kudumisha mauaji yake dhidi ya raia wa kawaida wa Yemen. Katika uwanja huo, ndege za muungano vamizi wa Saudia Jumamosi ya jana na katika radiamali yake kufuatia kutunguliwa ndege yake ya kisasa ya Tornado zilifanya mashambulizi makali katika eneo la Al Maslub na viunga vya eneo ilipotunguliwa ndege hiyo, ambapo katika hujuma hizo za kinyama zaidi ya watu 30 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa. Mohammad Abdul-Salam, Msemaji wa Harakati ya Wananchi ya Answarullah akitoa radiamali yake kufuatia shambulizi hilo amesema: "Kila mara muungano vamizi wa Saudia unapokabiliwa na vipigo katika ulingo wa vita, huwa unafanya jeuri na wendawazimu kwa kuwalenga raia wasio na hatia." Shambulizi hilo dhidi ya raia limethibitisha wazi kushindwa Saudia katika vita vyake vya kichokozi dhidi ya Yemen, hata hivyo kukubali kushindwa na kisha kutangaza kumalizika vita hivyo ni suala chungu na la kuumiza kwa utawala wa Aal Saud.

Tags

Maoni