Feb 18, 2020 01:38 UTC
  • Tuhuma mpya za Uturuki dhidi ya Imarati

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Suleyman Soylu ameituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati au UAE) kuwa inahusika katika kuchochea fitina ndani ya nchi yake.

Soylu amesema: "Ankara imewakamata watu ambao Imarati imekuwa ikiwachochea ili waidhuru Uturuki." Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuku aidha amesema, baadhi ya waliokamatwa walikuwa wakieneza uvumi na fitina na nafasi ya Imarati imebainika wazi katika uhalifu huo.

Tuhuma za hivi karibuni za Uturuki dhidi ya serikali ya Imarati zinatolewa katika hali ambayo, huko nyuma pia serikali hizo mbili zimekuwa zikituhumiana. Hadi sasa Uturuki imeituhumu Imarati mara kadhaa kuwa inaingilia mambo  yake ya ndani. Katika upande wa pili pia Imarati nayo imekuwa ikiituhumu Uturuki kuwa inaingilia mambo yake ya ndani. Katika mitandao ya kijamii aidha wakuu wa Imarati wamekuwa wakidai kuwa viongozi wa zamani wa Uturuki walihusika katika kupora turathi za Waarabu katika mji wa Madina na kuzihamishia Istanbul. Hata hivyo tuhuma hizo zimeishia tu katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

Katika jaribilo lililofeli la mapinduzi nchini Uturuki mnamo Julai 15 mwaka 2016, wakuu wa Uturuki waliwasilisha nyaraka zinazoonyesha namna ambavyo Imarati ilitoa msaada wa kifedha kwa mrengo wa Fethullah Gulen, na wafanyampainduzi wengine ambao walikuwa wanataka kuiangusha serikali ya Rais Reccep Tayyip Erdogan.

Fethullah Gulen

Serikali ya Uturuki imeshawasilisha nyaraka kuhusu madai hayo sambamba na kuwakamata watu ambao wanatuhumiwa kuhusika katika kuwafikishia fedha wafanya mapinduzi. Baadhi wa weledi wa mambo katika nchi za Kiarabu wameunga mkono Uturuki kuhusu kuhusika Imarati katika kuvuruga mambo huko Uturuki. Kwa mfano Muhammad bin Mukhtar Al-Shanqiti mtaalamu wa masuala ya kisaisa na mhadhiri wa chuo kikuu nchini Qatar ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Wawakilishi wa ngazi za juu wa mrengo wa Gulen walisafiri nchini Imarati mara 22 kabla ya Julai 2016 kwa lengo la kupanga njama ya mapinduzi.
Mtaalamu huyo wa Qatar anaongeza kuwa :"Wapanga njama hao wa mapinduzi ya Uturuki walipokea msaada wa dola bilioni 3 kuanzia Oktoba 2015 hadi Julai 2016.

Fauka ya hayo Davir Hartz mwandishi wa gazeti la the Guardian la Uingereza aliandika mwaka 2016 kuwa: "Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu imekuwa ikiwapa msaada wa kifedha wafanya mapinduzi wa Uturuki."

Hartz ambaye aliwahi kuwa mhariri wa gazeti la Guardian anaendelea kusema kuwa: "Kabla ya kutekeleza njama ya mpainduzi, Imarati ilikuwa inawasiliana na wafanya mapinduzi kupitia Mohammad Dahlan, mwanachama wa ngazi za juu wa harakati ya Fath ya Palestina ambaye alikuwa na mawasiliano ya karibu na Fethullah Gulen."

Baada ya kufeli njama hiyo ya mapinduzi, Dahlan amekuwa akitajwa kuwa mshauri wa mrithi wa Ufalme wa Imarati.

Mohammad Dahlan

Kwa vyovyote vile, pamoja na kuwa Uturuki imekuwa ikichapisha nyaraka dhidi ya Imarati na pia utawala wa Saudia, tunapaswa kusema kuwa, serikali za Uturuki na Qatar katika miongo miwili iliyopita zimekuwa zikiunga mkono mrengo wa Ikhwanul Muslimin katika eneo la Asia Magharibi na Afrika Kaskazini. Hii ni katika hali ambayo Imarati, Saudia na waitifaki wao ni wapinzani wa mrengo huo na daima wamekuwa wakijaribu kuidhoofisha Ikwanul Muslimin. Kwa hivyo tunapaswa kusema kuwa, hitilafu za Uturuki na nchi hizo za Kiarabu hasa Imarati, Saudia na Misri zinatokana na kadhia ya Ikwanul Muslimin (Muslim Brotherhood). Harakati hiyo ina nguvu nchini Misri na Libya na inadaiwa kuwa Uturuki na Qatar zinataka kundi hilo lichukue madaraka katika nchi hizo.

Tags

Maoni