Feb 19, 2020 10:56 UTC
  • Vijana waliopewa mafunzo na Luteni Soleimani wamuenzi kamanda wao mjini Halab Syria

Kwa siku kadhaa sasa wananchi wa kaskazini mwa Syria wameghariki katika furaha baada ya kukombolewa kikamlifu mji wa Halab uliokuwa unakaliwa kwa mabavu na magenge ya kigaidi kwa miaka mingi. Mji huo wa Halab ambao ni muhimu mno kwa Syria hasa kiuchumi, kisiasa, kielimu na kiutamaduni, ulikombolewa kikamilifu Jumapili wiki hii.

Hata jana Jumanne pia, wananchi wa Halab walikesha kusherehekea ushindi huo wakiwemo wale waliokusanyika katika meidan ya Saadullah al Jabiri. 

Katika sherehe zao hizo, wananchi hao wa Syria wamesikika wakisema wazi kuwa hawatosahau kamwe mchango wa Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH katika ukombozi wa ardhi zao. 

Wananchi wa Halab Syria katika mikesha ya kushangiria kukombolewa kikamilifu mji wao na kufurushwa magaidi

 

Televisheni ya al Alam imewanukuu wachambuzi mbalimbali wa mambo wakisisitiza kuwa, mchango wa Kamanda Soleimani aliyeuliwa kidhulma na Marekani nchini Iraq, unaonekana wazi katika ukombozi wa ardhi za Syria hasa kwa vile alikuwa pamoja na wananchi na serikali ya Syria tangu mwanzoni kabisa mwa mgogoro wa miaka tisa sasa wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, vijana waliopata mafunzo chini ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani ndio wanaoendeleza njia yake sasa hivi na kufanikiwa kukomboa maeneo mengi sana ya Syria. 

Katika baadhi ya maeneo yaliyokombolewa huko Syria kumebandikwa picha kubwa za Luteni Jenerali Qassem Soleimani ikiwa ni katika kuenzi mchango wake mkubwa katika kuwakomboa wananchi wa Syria. 

Sehemu zilizosalia hivi sasa bila ya kufurushwa magaidi huko Syria, ni baadhi ya maeneo ya mkoa wa Idlib ambapo taarifa zinasema kuwa, zaidi ya nusu ya mkoa huo umeshakombolewa na sasa hivi wanajeshi wa Syria na waitifaki wao wanaendeleza mapambano ya kuyafurusha kikamilifu magenge ya kigaidi katika kila shibri ya ardhi ya Syria.

Tags

Maoni