Feb 19, 2020 11:41 UTC
  • Askofu wa Kanisa Katoliki Lebanon: Mpango wa Muamala wa Karne ni namna fulani ya kutangaza vita

Kiongozi wa Kanisa Katoliki kusini mwa Lebanon amesema kuwa, mpango wa kibaguzi wa Muamala wa Karne unakinzana wazi kabisa na amani na kuishi pamoja na kimsingi ni namna fulani ya kutangaza vita.

Elie Bechara Haddad askofu wa  maeneo ya Saida na Deir Al-Qamar kusini mwa Lebanon amesema hayo leo ambapo mbali na kulaani mpango wa Kimarekani-Kizayuni wa Muamala wa Karne amesema kuwa, mpango na muamala wowote ule ambao unakanyaga haki za taifa la Palestina hautafanikiwa bali utashindwa na kugonga ukuta.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki kusini mwa Lebanon amesema wazi kuwa, hakuna nukta yoyote ile ya pamoja iliyoko baina ya mtazamo na itikadi za dini ya Kikristo na malengo ya utawala dhalimu wa Israekl kuhusiana na kadhia ya Palestina.

Maandamano ya Wapalestina ya kupinga mpango wa kibaguzi wa Muamala wa Karne

Aidha askofu Saïda Elie Bechara Haddad ameongeza kuwa, taifa shupavu la Palestina katu halitasalimu amri mbele ya malengo machafu ya Marekani na utawala wa kibaguzi wa Israel.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Jumanne ya tarehe 28 Januari, Rais wa Marekani, Donald Trump alizindua mpango wa Muamala wa Karne akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu. 

Kwa mujibu wa mpango huo wa Marekani, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni; wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki tena ya kurejea katika ardhi za mababu zao na Palestina itamiliki tu ardhi zitakazosalia huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza. 

Tags

Maoni