Feb 21, 2020 06:42 UTC

Msemaji wa Majeshi ya Yemen amesema kuwa, sasa ndege za kivita za wavamizi wa nchi hiyo hasa Saudi Arabia hazina usalama tena katika anga ya Yemen baada ya kuzinduliwa mifumo mipya ya ulinzi wa anga wa nchi hiyo.

Televisheni ya Almasirah imemnukuu Brigedia Jenerali Yahya Saree akisema hayo jana na kuongeza kuwa, mifumo mipya ya kujilinda na mashambulizi ya anga ya Yemen imeimarishwa kwa teknolojia mpya za kisasa na ina zana zenye uwezo mkubwa katika kutungua ndege za kijasusi na za kivita.

Amesisitiza kuwa, sasa anga ya Yemen si salama tena kwa maadui na kwamba kuanzia sasa ndege za maadui zitalazimika kupiga mahesabu makubwa kabla ya kuamua kuingia kwenye anga ya Yemen.

Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen,  Brigedia Jenerali Yahya Saree

 

Msemaji huyo wa majeshi ya Yemen ameongeza kuwa, mifumo mipya ya ulinzi wa anga ya Yemen iko tayari kabisa kuingia kwenye kanali ya ulinzi wa taifa hilo la Kiarabu.

Matamshi hayo yamekuja baada ya jeshi la Yemen kufanikiwa kutungua ndege ya kisasa kabisa ya kivita aina ya Tornado mapema Jumamosi iliyopita wakati ilipokuwa ikifanya mashambulizi ya kiuadui katika mkoa wa al Jowf nchini Yemen. Kwa mujibu wa Kamanda Saree, ndege hiyo ilitunguliwa kwa makombora ya nchi kavu kwa anga yaliyozatitiwa kwa teknolojia ya kisasa.

Ndege ya kivita aina ya Tornado imeundwa kushirikiana nchi za Uingereza, Ujerumani na Italia.  Madola hayo ya kibeberu ya Ulaya yameipa Saudi Arabia ndege hizo ili ifanye mauaji ya Waislamu wa Yemen. Hata hivyo kutunguliwa ndege hiyo kumezidi kufelisha njama za maadui wa taifa hilo la Waislamu.

Maoni