Feb 22, 2020 02:46 UTC
  • Vikosi vya Yemen vyashambulia tena Aramco ya Saudia

Kwa mara nyingine tena vikosi vya jeshi la Yemen vimefanya mashamblizi kwa kutumia makombora dhidi ya taasisi za shirika kubwa zaidi la mafuta la Saudi Arabia la Aramco katika mkoa wa Madina, magharibi mwa Saudia.

Msemaji wa Majeshi ya Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree jana Ijumaa aliwahutubia waandishi wa habari katika mji mkuu Sana'a na kusema kuwa, vikosi vya makombora na ulinzi wa anga vya jeshi la nchi hiyo vimetekeleza operesheni iliyopewa jina la "Operesheni ya Tatu ya Mlingano" na kupiga kwa makombora taasisi za mafuta na vituo vingine muhimu vya Aal-Saud katika mji wa bandari wa Yanbu, yapata kilomita 165 magharibi mwa Madina.

Amesema makombora ya balestiki ya Yemen yamelenga kwa shabaha maeneo yaliyokusudiwa na kuisababishia hasara kubwa serikali ya Riyadh.

 Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema mashambulizi hayo ya vikosi vya Yemen dhidi ya taasisi za mafuta za Saudia ni muendelezo wa operesheni za ulipizaji kisasi kwa uvamizi na hujuma za muungano wa Saudia dhidi ya taifa hilo la Kiarabu. 

Vikosi vya Yemen vimetekeleza mashambulizi hayo siku chache baada ya Wayemen zaidi ya 30 wakiwemo watoto 19 kuuawa katika mashambulizi ya anga ya Februari 15 yaliyofanywa na ndege za kijeshi za muungano vamizi wa Saudia katika mkoa wa Jawf, kaskazini mwa Yemen. 

Shambulizi dhidi ya Aramco miezi michache nyuma lililoathiri uzalishaji mafuta Saudia kwa asilimia 50

Yahya Sarie amesisitiza kuwa jeshi la Yemen litaendeleza mapambano hadi litakapofanikiwa kukomboa ardhi yote ya nchi hiyo na kuwafukuza kikamilifu wavamizi wa kigeni. 

Maelfu ya raia wa Yemen wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi tangu Saudi Arabia na washirika wake walipoanzisha mashambulizi dhidi ya taifa la Yemen mwezi Machi mwaka 2015.   

 

Tags

Maoni