Feb 26, 2020 07:11 UTC
  • Matokeo ya vita vya siku mbili kati ya Israel na wanamuqawama wa Palestina

Vita kati ya makundi ya muqawama ya Palestina na utawala haramu wa Israel vimemalizika kwa usitishaji mapigano.

Vita hivyo vilianza baada ya uchokozi wa utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza na kuuvunjia heshima mwili wa kijana mmoja mwenye umri wa miaka 27 aliyeuawa shahidi na utawala huo katili, na kufuatia radiamali kali ya makundi ya muqawama ya Palestina. Vita hivyo vilidumu chini ya masaa 48, lakini vimekuwa na matokeo muhimu sana. Aidha vita hivyo vimethibitisha kwamba uwezo wa utawala wa Kizayuni wa kupigana vita na makundi ya muqawama ya Palestina umepungua na kufikia masaa 48 pekee. Novemba 2018 utawala huo ulipigana vita na wanamuqawama kwa siku nne, huku mwezi Mei mwaka jana ukipigana na makundi hayo kwa muda wa siku mbili pekee na katika vita vya hivi karibuni umepigana kwa muda wa chini ya masaa 48 tu. Vita hivyo pia vimethibitisha mlingano wa 'piga nikupige' kwa maana kuwa makundi ya muqawama ya Palestina si tu kwamba hayakurudi nyuma mkabala wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni, bali yametoa jibu kali dhidi ya utawala huo vamizi kiasi kwamba usiku wa kuamkia Jumanne ya jana na kwa muda wa saa moja yalivurumisha maroketi 25 kwenda ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Makomando wa Harakati za muqawama wa Palestina walioitia adabu Israel

Mlingano wa piga nikupige umeonyesha kwamba makundi ya Palestina yapo katika hali ya utayarifu mkubwa ambapo yanaweza kutoa jibu kali dhidi ya jinai yoyote ya utawala wa Kizayuni. Nukta nyingine ni kwamba, mlingano wa piga nikupige umedhihirisha udhaifu na madhara unayoyapata utawala huo pandikizi unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu. Ukweli ni kwamba kwa mara nyingine mlingano wa piga nikupige umethibitisha kwamba jeshi la utawala wa Kizayuni, sio jeshi lenye nguvu katika eneo la Asia Magharibi. Kuhusiana na suala hilo, Alon Ben-David, mchambuzi mashuhuri wa masuala ya kijeshi wa Israel amekiri kwamba, utawala wa Kizayuni umeshindwa kikamilifu kukabiliana na wanamuqawama wa Kipalestina. Amebainisha kwamba katika mapigano hayo na baada ya kumuua shahidi Baha Abu al-Ata, mmoja wa makanda wa ngazi za juu wa Harakati ya Jihadul-Islami, ndege za kivita za Israel hazikuweza kuzuia wimbi la makombora ya muqawama wa Palestina. Ama ujumbe mwingine wa vita hivyo, ni kuwekwa wazi ukubwa wa ugaidi wa utawala khabithi wa Kizayuni. Hii ni kusema kuwa baada ya makundi ya muqawa kutoa jibu kali, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni kwa mara nyingine alitishia kuwa utawala huo utawaua kigaidi viongozi wa muqawama wa makundi ya Kipalestina.

Wanamuqawama wa Kipalestina

Kwa mara ya mwisho utawala huo ulimuua kigaidi Baha Abu al-Ata, mmoja wa makanda wa ngazi za juu wa Harakati ya Jihadul-Islami, mwezi Novemba mwaka jana. Kabla ya hapo pia, Netanyahu alitishia kuwa angewaua kigaidi viongozi na makamanda wa Palestina. Nukta ya mwisho ni kwamba, vita hivyo vinaweza kuwa na matokeo muhimu kwa utawala wa Kizayuni, hususan kwenye suala la kuundwa serikali ijayo. Katika uwanja huo, Ayman Odeh, Mkuu wa Mrengo wa Pamoja wa Kiarabu (Hadash Party) ambaye pia ni mwakilishi wa Kiarabu katika bunge la utawala haramu wa Kizayuni (Knesset) amesema: "Katika uchaguzi ujao wa bunge hatutamuunga mkono Benjamin Netanyahu wala Benny Gantz katika kuwania nafasi ya uwaziri mkuu, kwa kuwa Gantz hataki kuhitimishwa uvamizi na kupatikana amani huku Netanyahu pia akiwa bado anaendeleza mashambulizi dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza. Na sisi hatutoshirikiana kamwe na serikali ambayo inalishambulia eneo la Gaza." Ukweli ni kwamba iwapo hapo kabla Netanyahu alitaraji kupata uungaji mkono kutoka mrengo wa Kiarabu ili kumuwezesha kuunda serikali, hivi sasa amepoteza nafasi hiyo baada ya kutekeleza mashambulizi ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Gaza na hivyo kuendeleza mzozo wa kisiasa ndani ya Israel. 

Maoni