Feb 27, 2020 12:55 UTC
  • UN yaitaka Saudia iheshimu haki za binadamu, iwaachie huru wanawake

Kamishna MKuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa kuendelea kukamatwa wapinzani wa serikali nchini Saudi Arabia hususan wanaharakati wanawake, sanjari na kukiukwa haki za binadamu.

Michelle Bachelet amebainisha wasiwasi huo leo Alkhamisi katika hotuba yake kwa Baraza la Haki za Binadamu la UN, ambapo ameitaka serikali ya Riyadh iwaachie huru wanaharakati hao wanawake inaowazuilia.

Amesema wanawake hao wametiwa mbaroni na kuzuiliwa kwa ajili tu ya kupigania haki zao za msingi na kutaka kufanyiwa marekebisho sera kandamizi na za kibaguzi dhidi yao.

Michelle Bachelet ameutaka utawala wa Aal-Saud uheshimu haki na uhuru wa kujieleza, kukusanyika kwa amani, sambamba na kuangalia upya hukumu dhidi ya wanaharakati wa kijamii, wakosoaji, wanazuoni na waandishi wa habari haswa wakati huu ambapo Saudia inapojiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kundi la G20 mwaka huu.

Ukatili wa watawala wa Saudia

Kamishna MKuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa, "pia natoa mwito wa kuwepo uwazi katika mchakato wa kesi zilizopo mahakamani, pamoja na kuwajibishwa waliohusika na mauaji ya Jamal Khashoggi."

Mauaji ya kutisha yaliyofanywa na maafisa wa Saudi Arabia wakiwemo wasaidizi wa karibu wa mrithi wa ufalme nchini humo, Muhammad bin Salman mwezi Oktoba mwaka 2018 dhidi ya mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa Riyadh, Jamal Khashoggi katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Istanbul huko Uturuki yametajwa kuwa mfano wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na utawala huo wa kifalme.  

Maoni