Mar 12, 2020 08:05 UTC
  • Mgogoro baina ya Morocco na Imarati wapamba moto

Uhusiano wa kidiplomasia baina ya Morocco na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) umeingia katika mgogoro mkubwa baada ya Abu Dhabi kukataa kutuma balozi mpya mjini Rabbat, na Morocco nayo imeamua kushusha chini kabisa kiwango cha uhusiano wake wa kidiplomasia na Imarati.

Gazeti la Maghreb Intelligence limeripoti habari hiyo na kuvinukuu vyombo vya habari vya Morocco vikitangaza kuwa, hivi sasa kumezuka mgogoro mkubwa wa kidiplomasia baina ya nchi hiyo na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Vyombo hivyo vya habari vimeripoti kuwa, serikali ya Morocco imemwita nyumbani balozi wake nchini Imarati, Mohammad Ayat Waili,  na kufunga balozi zake ndogo katika miji ya Abu Dhabi na Dubai bali hata mwambata wa kijeshi wa Morocco nchini Imarati naye amerejea nyumbani bila ya kuieleza serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Viongozi wa Morocco wamesema wamechukua uamuzi huo kutokana na dharau na vitendo vya kiuadui vya viongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu kiasi kwamba hadi hivi sasa nchi hiyo imeshindwa kutuma balozi wake mjini Rabat. 

Bendera za Morocco na Imarati

 

Masuala ya kidiplomasia ya Umoja wa Falme za Kiarabu huko Morocco yanafanywa na idara moja ndogo tu suala ambalo limewakasirisha sana viongozi wa Rabat ambao wanakihesabu kitendo hicho cha Imarati kuwa ni dharau na jeuri kubwa kwa Morocco.

Habari nyingine zinasema kuwa, Morocco imefunga ubalozi na balozi zake zote ndogo nchini Imarati, hata washauri wa kidiplomasia pia imewarudisha nyumbani na kubakisha wafanyakazi wachache tu wa ngazi za chini kushughulikia mambo ya dharura inapobidi.

Hadi inaripotiwa habari hii, viongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu walikuwa hawajachukua hatua zozote za kujibu hatua hiyo kali ya Morocco.

Tags

Maoni