Mar 25, 2020 02:28 UTC
  • Ishara za kupata ushindi Serikali ya Wokovu wa Kitaifa katika vita nchini Yemen

Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen amesisitiza wakati huu wa kukaribia kutimia mwaka wa tano wa vita vya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen kwamba, nchi hiyo si tu kwamba, haijasalimu amri mbele ya muungano huo vamizi bali hii leo ipo katika nafasi ya kupata ushindi.

Vita vya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen vilianza tarehe 26 Machi 2015 na kesho Jumatano tarehe 26 Machi vinaingia mwaka wake wa sita. Katika kipindi hiki cha kukaribia kutimia mwaka wa tano wa vita hivyo, kuna ishara mbalimbali zinazoonyesha kuwa, Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen inayoundwa na Harakati ya Ansraullah na waitifaki wake imewapiku washindani wake katika matukio ya nchi hiyo.

Katika upande wa kisiasa, Machi mwaka 2015, Saudi Arabia ilianzisha vita dhidi ya Yemen kwa shabaha ya kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdurabbuh Mansur Hadi, Rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kisha kukimbilia usalama wake nchini Saudia. Hivi sasa baada ya kupita miaka mitano si tu kwamba, Mansur Hadi amefanikiwa kurejea mjini Sana’a, bali hata katika mji wa Aden ambako ndiko makao makuu ya serikali yake iliyojiuzulu pia ana mshirika na mshindani muhimu nalo ni Baraza na Mpito la Kusini lenye mfungamano na Imarati.

Kimsingi ni kuwa, nguvu na uwezo wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen ukiilinganisha na mwaka 2015 inaonekana imedhooika mno na vita vya muungano vamizi wa Saudia vimekuwa na nafasi katika hili. Katika upande mwingine, mzozo wa madaraka baina ya serikali iliyojiuzulu na Baraza la Mpito la Kusini umeshadidi mno katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kiasi kwamba, baadhi ya asasi za uongozi zilizoko chini ya usimamizi wa Baraza la Mpito la Kusini, Ansarulllah na waitifaki wake wameunda Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen katika mji mkuu Sana’a ambayo inahesabiwa kuwa taasisi yenye uratibu zaidi wa kisiasa kwa sasa katika nchi hiyo.

Katika uga wa operesheni za kijeshi, hali ya mambo hii leo nchini Yemen katu haiwezi kulinganishwa na mwaka 2015 wakati Saudia na washirika wake walipoanzisha hujuma ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen anasema kuwa, Yemen ilikabiliwa na idadi kubwa ya mashambulio ya anga katika historia ya vita duniani. Ameongeza kuwa, vituo vya kiufundi vya vikosi vya Yemen vimerekodi mashambulio 275,882 ya vikosi vya vamizi vinavyoongozwa na utawala wa Aal Saud.

Pamoja na hayo, baada ya kupita miaka 5 ya vita hivyo, Ansarullah na waitifaki wake wanadhibiti asilimia 70 ya maeneo ambayo ni makazi ya watu nchini Yemen.

Hujuma za Saudi Arabia dhidi ya Yemen zinavyosababisha uharibifu

Fauka ya hayo, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Jeshi la Yemen na Kamati za Wananchi zimetekeleza operesheni nne za kijeshi zilizokuwa na mafanikio na kuweza kubadilisha mahesabu hali ambayo imeufanya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia urejee nyuma. Operesheni hizo zimeusababishia hasara kubwa muungano vamizi wa Saudia.

Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen anasema kuwa, hadi sasa zaidi ya vifaru, magari ya deraya na mabuldoza 8,487 ya muungano vamizi yameangamizwa. Kupata hasara muungano huo wa kijeshi kumeulazimisha muungano huo wa kijeshi utiliane saini na baadhi ya mataifa mikataba ya kununua silaha nyingi zenye thamani ya mabilioni ya dola. Kabla ya hapo zaidi ya ndege 371 za kijeshi za muungano vamizi zikiwemo za apache na ndege 318 za kijasusi zilitunguliwa na makombora ya anga ya Yemen. Aidha zaidi ya askari na maafisa wa kijeshi 10,000 wa Aal Saud na zaidi ya askari 240 wa Imarati wameuawa au kujeruhiwa katika vita nchini Yemen.

Mafanikio ithbati tosha kwamba, mwaka wa tano wa vita nchini Yemen ulikuwa wa ushindi mtawalia kwa jeshi na kamati za wananchi wa Yemen na kuchezea vipigo mara kwa mara muungano vamizi wa Saudia na unahesabiwa kuwa mwaka muhimu zaidi katika vita hivyo; hasa kwa kuzingatia kwamba, mwaka huu umethibitisha kuongezeka uwezo wa jeshi na kamati za wananchi wa kumzuia adui kufanya mashambulio na hivyo kubadilisha kikamilifu uwiano na mlingano wa nguvu katika nchi hiyo.

Maoni