Mar 26, 2020 03:51 UTC
  • Matokeo ya kikao cha mawaziri wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi kilichohudhuriwa na Qatar

Kikao cha dharura cha mawaziri wa fedha wa nchi wanachama katika Baraza la ushirikino wa Ghuba ya Uajemi kilifayika Jumanne ya tarehe 24 Machi kupitia njia ya video kwa shabaha ya kuchunguza taathira za kifedha na kiuchumi za maambukizi ya virusi vya corona.

Kikao hicho kimemshirikisha pia Waziri wa Fedha wa Qatar. Japokuwa baadhi wachambuzi wamekutaja kushiriki waziri wa Qatar katika mkutao huo uliofanyika kwa njia ya video kuwa ni jambo lenye umuhimu, lakini inatupasa kukumbusha hapa kuwa, Doha pia ilishiriki katika mkutano kama huo uliofanyika Disemba mwaka jana; kwa msingi huo hii si mara ya kwanza kwa Qatar kushiriki vikao vya baraza hilo tangu mwezi Juni mwaka 2017. 

Nukta nyingine ya kuashiriwa ni kwamba, kushiriki kwa Qatar katika mkutano wa Jumanne iliyopita wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (GCC) linalojumuisha nchi za Saudi Arabia, Kuwait, Bahrain, Oman, Imarati na Qatar si ishara ya mabadiliko katika uhusiano nchi hiyo na baraza hilo, kwani mabadiliko kama hayo yatatokea pale Amir wa Qatar mwenyewe atakaposhiriki vikao vya viongozi wa jumuiya hiyo. Mkutano wa Disemba mwaka jana wa viongozi hao ulihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Qatar na si Amir wa nchi hiyo, na mkutano wa juzi Jumanne ulihudhuriwa na Waziri wa Fedha tena kwa njia ya video. 

Mfamle Salman wa Saudia (kushoto) na Amir wa Qatar

Nukta nyingine ni kwamba, virusi vya corona ndiyo iliyokuwa sababu kuu ya kuitishwa mkutano wa juzi wa mawaziri wa fedha wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi. Kwa maneno mengine ni kuwa, "tishio la pamoja" ndiyo sababu ya kuitishwa mkutano huo uliohudhuriwa na waziri wa Qatar. Suala hili lina maana kwamba, miongoni mwa sababu kuu za kutoshiriki kiongozi na Amir wa Qatar katika mikutano ya mwaka 2017, 2018 na 2019 ya viongozi wa GCC ni kutokuwepo tishio la pamoja. Kwa hakika si tu kwamba hakukuwepo tishio la pamoja baina ya Qatar na nchi nyingine wanachama wa GCC, bali pia tunaweza kusema kuwa, mienendo ya nchi tatu wanachama wa kundi hilo ambazo ni Saudi Arabia, Imarati na Bahrain ni tishio kubwa kwa Qatar. Kwa sababu hiyo kiongozi wa Qatar Sheikh Tamim anasema kuwa, sharti la kushiriki kwake katika mikutano ya baraza hilo ni kufutwa vikwazo na kukomeshwa mzingiro wa Riyadh, Abu Dhabi na Manama dhidi ya nchi yake.

Nukta nyingine ya kuashiria ni kwamba, ni kweli kwamba corona ni tishio la dunia nzima, lakini hapana shaka kuwa, tishio hilo ni kubwa zaidi kwa baadhi ya nchi kuliko nyingine. Kwa mfano tu, Saudi Arabia kati ya nchi za Kiarabu wanachama wa kundi la GCC, ndiyo iliyoathiriwa zaidi na virusi vya corona kuliko wanachama wengine. Hii ni kwa sababu, sambamba na kasi kubwa ya maambukizi ya corona, bei ya mafuta katika masoko ya kimaaifa imeteremka na kufikia kiwango cha chini kabisa katika miaka ya hivi karibuni. Pipa moja la bidhaa hiyo sasa linauzwa dola 20. Wakati huo huo Saudi Arabia imetumbukia katika vita vya mafuta na Russia na vilevile inaendelea kunasa katika kinamasi cha vita vyake dhidi ya taifa la Yemen, na yote hayo yanaathiri vibaya na kwa kiwango kikubwa uchumi wa serikali ya Riyadh.

Salman na mwanaye, Muhammad

Maajabu ya dunia ni kwamba, Riyadh ambayo imekuwa ikifanya jitihada za kuishinikiza Qatar kiuchumi na kulemaza uchumi wa nchi hiyo, sasa inaketi meza moja na viongozi wa ngazi za chini wa nchi hiyo kwa ajili ya kujadili taathira mbaya za kiuchumi za virusi vya corona!

Mkutano wa Jumanne iliyopita wa baraza la GCC na taarifa yake ya mwisho vimeonyesha kuwa, kama ambavyo zinatambua corona kuwa ni tishio la pamoja, nchi za eneo la magharibi wa Asia iwapo zitarekebisha mitazamo yao kuhusiana na vitisho na changamoto muhimu za eneo hilo na kuwa na mtazamo wa pamoja kuhusiana na vitisho kama ugaidi, mitazamo mikali na sera za mabavu, zinaweza kutengeneza mazingira mazuri zaidi ya kuimarisha ushirikiano na kuondoa hitilafu baina yao.   

 

Maoni