Mar 26, 2020 07:59 UTC
  • Yemen yakaribisha uamuzi wa muungano wa kijeshi wa Saudia wa kuafiki kusitisha mapigano

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amekaribisha uamuzi uliotangazwa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia wa kuafiki pendekezo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la kusitisha vita na kupunguza mivutano nchini Yemen ili kusaidia mapambano dhidi ya maambukizi ya kirusi cha corona.

Muhammad Ali Al-Houthi ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter akieleza kwamba: Tunakaribisha tangazo la muungano unaoongozwa na Saudi Arabia wa kuunga mkono usitishaji vita, kupunguza mivutano na kuchukua hatua za kivitendo za kujenga hali ya kuaminiana baina ya pande mbili katika masuala ya kiutu na kiuchumi; wanaochubiri wananchi wa Yemen ni kutekelezwa kivitendo usitishaji vita huo.

Msemaji rasmi wa vikosi vya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia Turki al-Maliki alitangaza jana kuwa, kamandi ya vikosi vya pamoja vya muungano huo, inaafiki na inaunga mkono uamuzi wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen ya kukubali wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitishwa vita nchini Yemen na kukabiliana na athari za maambukizi ya kirusi cha corona.

Kabla ya tamko hilo la al-Maliki serikali ya Yemen iliyojiuzulu inayoongozwa na Abd Rabbuh Mansur Hadi ilitoa taarifa ya kukaribisha pendekezo la Umoja wa Mataifa la kusitisha mapigano nchini humo.

Siku ya Jumatatu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kusitishwa mapigano haraka kote duniani na kuelekezwa nguvu zote katika adui mkubwa wa sasa ambaye ni virusi vya Corona, COVID-19.

Uvamizi wa kijeshi wa muungano unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen umeingia katika mwaka wake wa sita huku utawala wa Riyadh ukiwa umeshindwa kufikia hata moja katika malengo yake, ghairi ya kusababisha maafa makubwa tu ya roho za watu na kuteketeza miundombinu ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.../

Tags

Maoni