Apr 06, 2020 02:33 UTC
  • Harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq yatahadharisha juu ya malengo ya Marekani ya kubakia kwa muda mrefu nchini Iraq

Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa wa Harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq ya nchini Iraq ametahadharisha juu ya mipango ya Marekani ya kutaka kubakia kwa muda mrefu nchini humo.

Sa'adu Al-Sa'adi, Mjumbe wa Harakati ya Kisiasa ya Asa'ib Ahl al-Haq nchini Iraq amesem kuwa, harakati za sasa za Marekani nchini humo zinaonyesha kuwa wavamizi hao wanakusudia kutia kambi zaidi na sio kuondoka katika ardhi ya Iraq. Al-Sa'adi amesema kuwa madai ya kuondoka askari wa Marekani nchini Iraq sambamba na kusimikwa ngao ya makombora ya Patriot, ni mambo yanayokinzana na kuongeza kuwa daima taifa la Iraq limekuwa likipinga uwepo uvamizi wa Wamarekani katika ardhi ya nchi hiyo.

Sehemu ya askari vamizi wa Marekani nchini Iraq

Hii ni katika hali ambayo Alkhamisi iliyopita Gabriel Suma, Mshauri wa Rais Donald Trump wa Marekani alithibitisha habari ya kufika katika kambi za jeshi la Marekani nchini Iraq ngao ya makombora ya Patriot. Sa'adu Al-Sa'adi, Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Asa'ib Ahl al-Haq nchini Iraq ameashiria pia uingiliaji na mashinikizo ya wazi ya Marekani katika mwenendo wa kuundwa serikali ya Adnan al-Zurfi nchini Iraq na kusema, al-Zurfi amepuuza kikamilifu uamuzi wa bunge wa kuondoka askari wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa Adnan al-Zurfi aliteuliwa na Rais Barham Salih tarehe 17 Machi na kumtaka aunde serikali mpya, hata hivyo amekumbwa na upinzani mkali wa makundi ya kisiasa ya Kishia. Baadhi ya makundi hayo yanaamini kuwa al-Zurfi siye shakhsia wa kujitegemea na aliye na misimamo huru, bali anafungamana na pande za kigeni hususan Marekani.

Tags

Maoni