Apr 06, 2020 07:44 UTC
  • Shirika la ujasusi la Israel Mossad lashukiwa kuhusika na mauaji ya kamanda wa Hizbullah

Duru za Lebanon zimesema, shirika la ujasusi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Mossad na vibaraka wake ndio wanaoshukiwa kuhusika na mauaji ya kamanda wa Hizbullah Muhammad Ali Yunus.

Siku ya Jumamosi, watu wasiojulikana walimuua shahidi Muhammad Ali Yunus, mmoja wa makamanda wa harakati ya muqawama ya Lebanon Hizbullah huko kusini mwa nchi hiyo.

Kamanda huyo wa Hizbullah alikuwa akiongoza kikosi cha kuwafuatilia vibaraka na mamluki wanaojipenyeza ndani ya harakati hiyo.

Kutokana na jinsi mauaji ya Muhammad Ali Yunus yalivyofanywa, tovuti ya habari ya al-Junubiyyah ya Lebanon imeripoti kuwa, vikosi vya muqawama wa Kiislamu vya Hizbullah vimeweka uzio wa kiusalama mahali pa tukio hilo na tayari vimeshapata vidokezo kuhusu wahusika wa mauaji hayo kutokana na faili nyeti na muhimu ambalo Yunus alikuwa akilishughulikia.

Gazeti la Al-Qudsul-Araby limeandika kuwa, sababu ya kuuliwa kamanda huyo wa Hizbullah bado haijajulikana lakini taarifa iliyotolewa na Hizbullah ya Lebanon ya kutoa pongezi na mkono wa pole kwa kuuawa shahidi kamanda huyo inaashiria kuwepo uhusiano kati ya mauaji yake na operesheni ya kiusalama.

Mwili wa shahidi Muhammad Ali Yunus ulisindikizwa na kuzikwa jana jioni nchini Lebanon.../ 

Tags

Maoni