Apr 08, 2020 07:46 UTC
  • Vuta nikuvute juu ya uwaziri mkuu wa al-Zurfi huku makundi ya Kiiraqi yakikaribia kufikia mwafaka

Kufuatia upinzani mkali wa makundi ya Kishia kwa pendekezo la kumfanya Adnan al-Zurfi waziri mkuu mpya wa Iraq, waungaji mkono wa waziri mkuu huyo mteule aliyepewa jukumu la kuunda serikali wameyumba kimsimamo na hivi sasa makundi ya kisiasa nchini humo yanakaribia kufikia mwafaka wa kumpendekeza shakhsia mwingine mpya wa kushika wadhifa huo.

Jana Jumanne, ziliripotiwa habari nyingi kuhusu kupendekezwa waziri mkuu mwingine mpya wa Iraq. Maudhui kuu ya habari hizo ni kukaribia makundi ya Kiiraqi kufikia mwafaka wa kuwa na kauli moja ya kumpinga Adnan al-Zurfi, waziri mkuu mteule aliyekabidhiwa jukumu la kuunda serikali. Vyombo vya habari viliripoti kuwa, makundi ya kisiasa ya Kishia, yanayojumuisha harakati ya Al-Hikmah inayoongozwa na Ammar al-Hakim, Muungano wa Al-Fat'h unaoongozwa na Hadi al-Ameri, Muungano wa Utawala wa Sheria ambao kiongozi wake ni Nouri al-Maliki, Muungano wa Sairun unaoongozwa na Muqtada Sadr, Chama cha al-Fadhilah ambacho kiongozi wake ni Muhammad al-Yaaqubi pamoja na Muungano wa al-Aqd unaoongozwa na Falih al-Fayyadh, yamesisitiza kuwa yanapinga Adnan al-Zurfi kuwa waziri mkuu wa Iraq na yamekubaliana kumpendekeza Mustafa al-Kadhimi kushika wadhifa huo.

Adnan al-Zurfi

Inasemekana kuwa, mirengo wa Kikurdi na muungano wenye nguvu wa Kisuni wa Al-Iraqiyyah unaoongozwa na Spika wa Bunge Muhammad al-Halbousi nayo pia ina mtazamo sawa na wa makundi ya Kishia kuhusu kumuarifisha Mustafa al-Kadhimi. Kuhusiana na suala hilo, Shirwan Mirza, mbunge wa chama cha Muungano wa Kizalendo wa Kurdistan ya Iraq ametangaza uungaji mkono wa Wakurdi kwa uamuzi rasmi na wa mwisho utakaopitishwa na makundi ya kisiasa ya Kishia na akaeleza kwamba, al-Zurfi yuko katika mazingira magumu kwa sababu anapingwa na karibu makundi sita ya kisiasa ya Kishia, hivyo atafikwa na hatima sawa na iliyomfika Muhammad Allawi.

Ijapokuwa kabla ya hapo, Adnan al-Zurfi alikuwa ametangaza kuwa hatoghairi kuunda serikali; na akasisitiza kuhusu ulazima wa kuitishwa kikao cha bunge kwa ajili ya kuipigia kura serikali mpya atakayounda, lakini hapo jana ziliripotiwa habari kadhaa kuhusu uwezekano wa yeye kughairi uamuzi wa kuunda baraza jipya la mawaziri. Kuhusiana na suala hilo, Falah al-Khaffaji, mbunge wa mrengo wa an-Nasr katika bunge la Iraq alisema, ikiwa utafikiwa mwafaka wa kuwa na kauli moja vyama vya Kishia kuhusu kumbadilisha Adnan al-Zurfi, mwanasiasa huyo ataachana na mpango wa kuunda serikali mpya. Ukweli ni kwamba, kukaribia kufikia mwafaka makundi ya Kishia wa kupinga uwaziri mkuu wa Adnan al-Zurfi, kumedhoofisha nafasi yake ya kisiasa na waungaji mkono wake.

Kutangaza kuwa tayari kujiengua endapo utafikiwa mwafaka kati ya makundi ya Kishia, kumetokana zaidi na hofu ya kushindwa waungaji mkono wa al-Zurfi. Kughairi kuunda serikali kunaweza kukatumiwa kipropaganda pia ili kuonyesha kuwa Al-Zurfi mwenyewe na waungaji mkono wake wamefadhilisha kulinda umoja wa makundi ya Kishia badala ya utengano. Na hii ni pamoja na kwamba, mnamo Machi 17, pale Adnan al-Zurfi alipokabidhiwa jukumu la kuunda serikali na Rais Barham Salih, yeye na waungaji mkono wake walifanya kila njia kufanikisha jambo hilo bila kujali upinzani mkubwa wa makundi ya Kishia; na hata balozi wa Marekani nchini Iraq pia alitoa kama kawaida yake matamshi ya kuingilia masuala ya ndani ya Iraq, kwa kutaka al-Zurfi aunde serikali mpya ya nchi hiyo.

Rais Barham Salih wa Iraq

Mbali na sababu ya ukuruba wake na Marekani, sababu muhimu zaidi iliyoyafanya makundi ya Kishia yapinge uwaziri mkuu wa Adnan al-Zurfi ni namna alivyoarifishwa na Rais Barham Salih. Kulingana na Katiba ya Iraq, waziri mkuu inapasa atoke kwenye mrengo mkubwa zaidi bungeni, lakini Rais Barham Salih hakuzingatia hilo, bali yeye mwenyewe alimkabidhi al-Zurfi jukumu la kuunda baraza jipya la mawaziri. Jambo hilo lililalamikiwa vikali na makundi ya Kishia nchini Iraq ambayo yanaamini kuwa, hatua hiyo ya ukiukaji sheria inaweza ikageuka katika siku za usoni kuwa utaratibu wa kisiasa uliozoeleka. Kwa sababu hiyo inapasa upingwe na kuzuiwa tokea hivi sasa.

Hata kama mwafaka rasmi bado haujafikiwa kati ya makundi yote ya kisiasa nchini Iraq katika kupinga uwaziri mkuu wa Adnan al-Zurfi na waziri mkuu mwengine mpya bado hajatangazwa, lakini nukta muhimu ni kwamba, Iraq itakivuka kipindi hiki kwa gharama ndogo zaidi za mpasuko na utengano wa kisiasa baina ya makundi na mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo.../

 

Tags

Maoni