Apr 09, 2020 02:44 UTC
  • Yemen yalaani jinai ya Wasaudia ya kushambulia vituo vya karantini ya wagonjwa wa Corona

Kamati Kuu ya Kukabiliana na Virusi vya Corona nchini Yemen, imelaani vikali mashambulizi ya wavamizi wa Saudi Arabia dhidi ya vituo vya karantini na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa Corona nchini humo.

Ndege za muungano vamizi wa Saudia zimeshambulia kituo kilichoandaliwa kwa ajili ya wagonjwa wa Corona kwenye shule ya Al-Muhajabah katika mkoa wa Al Bayda na kadhalika eneo lililoandaliwa kwa ajili ya kuwaweka karantini madereva wa malori, karibu na eneo la Afar. Aidha kamati hiyo imesema kuwa, mashambulizi ya wavamizi yanatekelezwa kwa lengo la kusambaza ugonjwa wa Corona ambao hapo kabla haukuwepo ndani ya nchi hiyo.

Saudia yavuruga juhudi za kuzuia corona nchini Yemen.

Taarifa ya kamati ya kukabiliana na Corona nchini Yemen imeeleza kwamba, kabla ya hapo pia ndege za muungano vamizi wa Saudia zilitekeleza shambulizi karibu na eneo la karantini kwa ajili ya wagonjwa wa Corona katika eneo la Kamaran la mkoa wa Al Hudaydah. Aidha kamati hiyo imefafanua kuwa, kabla ya hapo askari wa muungano vamizi na vibaraka wao sambamba na kuizingira Yemen na kuwafukuza Wayemen nchini Saudia, wamekuwa wakifanya njama za kusambaza virusi vya Corona ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu. Wakati huo huo siku ya Jumanne Msemaji wa Jeshi la Yemen alisema kuwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita ndege za muungano vamizi wa Saudia zimetekeleza karibu mashambulizi 300 katika mikoa tofauti ya nchi hiyo.

Tags

Maoni