Apr 09, 2020 08:23 UTC
  • Radiamali ya ofisi ya Rais wa Afghanistan kwa hatua ya Taliban ya kusitisha mazungumzo

Ofisi ya Rais wa Afghanistan imelikosoa kundi la Taliban kwa hatua yake ya kusitisha mazungumzo yake na serkali hiyo.

Siddiq Siddiqi, msemaji wa ofisi ya rais wa Afghanistan ameandika ujumbe kwenye ukurasa wa Twitter akilituhumu kundi la Taliban kuwa linazusha visingizio kwa ajili ya kuanzisha mazungumzo na akatangaza kuwa, hakuna sababu wala kisingizio chochote ambacho kundi la Taliban linaweza kukitumia ili kuakhirisha mazungumzo kati yake na serikali ya Afghanistan.

Siddiq Siddiqi ameongeza kuwa: Ikiwa kundi la Taliban lina nia ya dhati ya kufikia suluhu, hakuna sababu nyingine yoyote ya kuakhirisha mazungumzo, kwa sababu serikali ya Afghanistan imechukua hatua muhimu kadhaa kwa ajili ya kufikia suluhu.

Tangu wiki iliyopita, wawakilishi wa kundi la Taliban walikuwa kwenye mazungumzo na serikali mjini Kabul ya kujadili namna ya kuwaachia huru wafungwa wa pande mbili, lakini msemaji wa ofisi ya kisiasa ya Taliban Suhail Shaheen amenukuliwa akisema, mazungumzo baina yao na serikali ya Afghanistan kuhusu kuachiwa huru wafungwa yamesimamishwa.

Msemaji wa Taliban, Suhail Shaheen

Kusimamishwa mazungumzo ya serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban yanayojadili ajenda ya kuachiwa huru wafungwa wa pande mbili kumejiri baada ya kundi hilo kuituhumu serikali ya Kabul kuwa inakwamisha mpango wa kuwaachia huru wafungwa wake kwa lengo la kulishinikiza katika mchakato wa mazungumzo hayo.

Baada ya Marekani na Taliban kufikia makubaliano mnamo Februari 29 huko mji mkuu wa Qatar, Doha, Rais Muhammad Ashraf Ghani aliahidi kuwaachia huru wafungwa wa Taliban, ambapo kwa mujibu wa ahadi hiyo wafungwa 1,500 miongoni mwa wafungwa wote wa kundi hilo ilikuwa waachiwe huru kabla ya kufanyika mazungumzo baina ya Waafghani, na wengine waliosalia ilikuwa waachiliwe huru wakati mchakato wa mazungumzo hayo utakapokuwa ukiendelea.

Uamuzi huo wa Ashraf Ghani ulikabiliwa na radiamali kali na ya haraka ya upinzani wa jamii ya Afghanistan hususan wa shakhsia wa kisiasa. Wakosoaji waliuelezea uamuzi huo kuwa ni utoaji fursa na upendeleo usio na hoja ya kuutetea uliofanywa hata kabla ya mazungumzo baina ya Waafghani, na ambao unaweza kupelekea kudhoofiika nafasi ya serikali katika mchakato wa mazungumzo hayo.

Makutano na vyombo vya habari baada ya mazungumzo ya Doha

Ahadi ya Ashraf Ghani ya kuwaachia huru wafungwa wa Taliban ambayo ilikuwa moja ya mambo yaliyoahidiwa na Marekani katika mkataba wa suluhu wa Doha iliosaini na kundi hilo ilitangazwa na Rais wa Afghanistan kwa mashinikizo ya Washington.

Ijapokuwa siku moja tu baada ya kusainiwa maafikiano ya Doha Ashraf Ghani alitamka kuwa Marekani haina ustahiki wa kujipa mamlaka ya kutoa ahadi ya kuachiwa huru wafungwa wa Taliban na akapinga suala hilo, lakini kwa mashinikizo ya Ikulu ya Washite House mwishowe alikubali kipengee hicho kiambatanishwe kwenye makubalinao hayo.

Kutokana na kuongezeka ukosoaji wa ndani kwa uamuzi wa Ashraf Ghani wa kuafiki kuachiliwa huru wafungwa wa kundi la Taliban, katika anga ya mivutano mikali iliyoibuka ndani ya Afghanistan baada ya yeye na Abdullah Abdullah kila mmoja kula kiapo cha urais kulikoshadidisha mgogoro wa kisiasa nchini humo, hata zoezi la kuwaachia huru wafungwa 1,500 wa Taliban lililokuwa litekelezwe kabla ya kuanza mazungumzo baina ya mirengo ya Waafghani, nalo pia liliakhirishwa.

Ashraf Ghani (kulia) na Abdullah Abdullah

Kwa kutilia maanani hali ilivyo hivi sasa nchini Afghanistan, inavyoonekana Ashraf Ghani amekabidhi uamuzi wa kuwaachia huru wafungwa wa Taliban kwa ujumbe unaoiwakilisha serikali katika mazungumzo na kundi hilo, ili kwa njia hiyo aweze kupunguza sehemu ya mashinikizo ya ndani yanayomwandama na hivyo kuubebesha ujumbe huo dhima ya athari zozote hasi zinazoweza kusababishwa na uamuzi huo.

Kubadilika mbeba dhima ya maamuzi kuhusu kuwaachia huru wafungwa wa Taliban na kuwa ni ujumbe wa wawakilishi wa serikali ya Afghanistan badala ya Ashraf Ghani kumewafanya maafisa waandamizi wa kundi hilo waichukulie hatua ya kuakhirisha kutekeleza ahadi ya mwanzo iliyotolewa na Ashraf Ghani kuwa ni aina fulani ya upotezaji wakati na ukwamishaji wa mchakato wa kufikia suluhu.

Ni kutokana na dhana hiyo, ndipo kundi la Taliban na kwa lengo la kuishinikiza serikali ya Afghanistan, likaamua kusimamisha mazungumzo ya kujadili mpango wa kuwaachia huru wafungwa baina yake na wawakilishi wa Kabul.../

 

Maoni