Apr 09, 2020 11:09 UTC
  • Saudia yatangaza kusitisha vita Yemen kisha yakiuka tangazo hilo

Muungano wa kivita unaaongozwa na Saudi Arabia, ambao Jumatano mchana ulitangaza kile ulichodai ni 'usitishaji vita' katika hujuma yake ya kinyama dhidi ya Yemen, ulikiuka tangazo lake hilo Jumatano usiku kwa kudondosha mabomu katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo.

Siku ya Jumatano, muungano huo vamizi ulitangaza kuwa ungesitisha hujuma zake za kijeshi nchini Yemen ili kuunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa za kumaliza hujuma ya Saudia ya miaka mitano Yemen, ambayo imepelekea makumi ya maelfu ya watu kuuawa na kueneza njaa na maradhi.

Msemaji wa muungano vamizi wa Saudia Kanali Turki al-Malki amedai kuwa tangazo la usitishwaji vita ni sehemu ya jitihada za kuzuia kuenea ugonjwa wa corona nchini Yemen. Alisema usitishwaji vita huo utaanza saa sita mchana Alhamisi kwa muda wa wiki mbili na unaweza kuongezwa. Lakini punde baad aya tangazo hilo, ndege za kivita za muungano huo wa Saudia zilidondosha mabomu katika maeneo ya Sa'ada, Amran na al-Bayda.

Kabla ya mashambulizi hayo, Harakati ya Ansarullah ilikuwa imesema tangaza hilo la usitishwaji vita la Saudia ni mbinu ya utawala wa Riyadh kujiondoa katika kinamasi cha Yemen bila kufedheheka sana. Muhammad al-Bukhaiti, mjumbe mwandamizi wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ameongeza kuwa, Saudia mara kwa mara hutangaza kusitisha vita lakini hukiuka mapatano hayo kila wakati. Aidha amesema maadamu mzingiro wa Saudia dhidi ya Yemen unaendelea vita haviwezi kumalizika.

Shule iliyoharibiwa katika hujuma ya Saudia dhidi ya Yemen

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia. 

 

Maoni