Apr 10, 2020 08:24 UTC
  • Kujiuzulu al-Zurfi na kufunguliwa njia ya kupatikana mshikamano wa kisiasa ndani ya Iraq

Baada ya kujiuzulu Adnan al-Zurfi, Rais Barham Salih wa Iraq amemteua Mustafa al-Kadhimi kuwa waziri mkuu mpya na kumpa jukumu la kuunda serikali.

Tarehe 17 Machi, Rais wa Iraq alimteua Adnan al -Zurfi kuwa waziri mkuu na kumkabidhi jukumu la kuunda baraza jipya la mawaziri.

Baadhi ya makundi ya kisiasa ya Iraq yalipinga uteuzi huo na kuanzisha kampeni ya kutafuta shakhsia mwingine wa kutaka apendekezwe kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.

Hatimaye Adnan al-Zurfi amelazimika kujiuzulu na kughairi kutekeleza jukumu alilokabidhiwa na Rais Barham Salih la kuunda serikali.

Suali la msingi linaloulizwa ni kwamba, ni akina nani waliopinga uwaziri mkuu wa Adnan al-Zurfi na walifanya hivyo kwa sababu gani hasa?

Adnan al-Zurfi

Muungano wa al-Fat'h unaoongozwa na Hadi al-A'meri na Muungano wa Utawala wa Sheria ambao kiongozi wake ni Nouri al-Maliki ni miongoni mwa mirengo muhimu zaidi ya kisiasa nchini Iraq iliyopinga uteuzi wa Adnan al-Zurfi. Upinzani wao haukutokana sana na nafasi ya kisiasa ya al-Zurfi, lakini utaratibu aliotumia Rais Barhma Salih kumuarifisha kuwa waziri mkuu ndio hasa ulioyafanya makundi hayo ya kisiasa yapinge uteuzi huo.

Kwa mtazamo wa makundi ya kisiasa ya Kishia, waziri mkuu inapasa ateuliwe kutoka mrengo mkubwa zaidi bungeni, lakini rais wa nchi hiyo alikiuka katiba kwa kumteua Adnan al-Zurfi bila kuzingatia mrengo mkubwa wa kisiasa katika bunge la Iraq.

Suali jengine linaloulizwa ni, kujiuzulu al-Zurfi na kuarifishwa Mustafa al-Kadhimi kuwa waziri mkuu mteule wa Iraq mwenye jukumu la kuunda serikali kutakuwa na matokeo gani?

Inavyoonekana, taathira chanya na muhimu zaidi ya kujiuzulu Adnan al-Zurfi ni kupatikana mshikamano baina ya makundi ya kisiasa ya Iraq; kwa sababu kuteuliwa kwake yalikuwa ni matokeo ya kukosekana mshikamano baina ya makundi ya kisiasa ya Kishia.

Mustafa al-Kadhimi

Utaratibu uliowekwa Iraq ni kwamba, Rais inapasa awe Mkurdi, Waziri Mkuu Mshia na Spika wa Bunge Msuni.

Baada ya kutambua hali ya mambo ilivyo, makundi ya Kishia ya Iraq, hususan katika kipindi cha siku kumi zilizopita, yamefanya jitihada za kuleta umoja na mshikamano baina yao. Katika muktadha huo, wakati muungano wa Sairun unaoongozwa na Muqtada Sadr na kwa kiwango fulani harakati ya Hikmah inayoongozwa na Ammar al-Hakim zilikuwa zimeunga mkono kuteuliwa kwa Adnan al-Zurfi, hatimaye makundi hayo mawili yameungana na mirengo ya Al-Fat'h na Utawala wa Sheria na kuunga mkono uwaziri mkuu wa Mustafa al-Kadhimi.

Haidar al-Abadi kiongozi wa muungano wa an-Nasr, ambao kiongozi wake bungeni ni Adnan al-Zurfi, na ambaye alikuwa ndiye muungaji mkono mkubwa wa mwanasiasa huyo, naye pia ameungana na makundi mengine ya Kishia kumpendekeza Mustafa al-Kadhimi kuwa waziri mkuu mpya wa Iraq.

Taathira nyingine chanya ya kujiuzulu al-Zurfi ni kuongezeka uwezekano wa kuundwa serikali na kuhitimishwa mkwamo wa kisiasa nchini humo.

Mwafaka juu ya suala la uwaziri mkuu wa al-Kadhimi haujahusisha makundi ya Kishia pekee, kwani hata makundi ya Kikurdi na Kisuni ya Iraq, nayo pia yamemjulisha Adnan al-Zurfi kuwa hayaungi mkono kuteuliwa kwake.

Ndiyo kusema kuwa al-Zurfi amepoteza kikamilifu fursa ya kuunda serikali. Nukta nyingine muhimu ni kuwa, wakati Muhammad Allawi alipofika bungeni ndipo alipobaini kuwa hakuna uwezekano wa yeye kuunda serikali, lakini Adnan al-Zurfi ametambua hivyo na kujiuzulu hata kabla ya kufika mbele ya bunge.

Rais Barham Salih (kushoto) akimkabidhi Mustafa al-Kadhimi (kulia) hati ya uteuzi na jukumu la kuunda serikali

Kutokana na uwaziri mkuu wa Muhammad al-Kadhimi kuungwa mkono na makundi saba ya Kishia (ya Al-Fat'h, Sairun, Utawala wa Sheria, Hikmah, Chama cha al-Fadhilah, ambacho kiongozi wake ni Muhammad al-Yaaqubi na muungano wa al-Aqd unaoongozwa na Falih al-Fayadh na pia muungano wa an-Nasr), pamoja na Wakurdi na muungano wenye nguvu wa al-Iraqiyyah unaoongozwa na Spika wa Bunge Muhammad al-Halbousi, hivi sasa Imwafaka wa kisiasa unakaribia kupatikana nchini Iraq ambao utahitimisha mkwamo wa kisiasa wa zaidi ya miezi minne sasa.

Mustafa al-Kadhimi mwenye umri wa 53 hana mfungamano na chama chochote cha siasa. Mwezi Juni 2016 aliteuliwa kuwa mkuu wa shirika la intelijensia la Iraq, cheo ambacho anakishikilia hadi hivi sasa.

Al-Kadhimi ana muda wa mwezi mmoja wa kuunda serikali mpya; na inavyoonekana makundi ya kisiasa nchini Iraq yatakuwa naye bega kwa bega katika kufanikisha mchakato huo.../

Tags

Maoni