Apr 10, 2020 10:40 UTC
  • Saudi Arabia na usitishaji vita nchini Yemen

Saudi Arabia imetangaza kuanza usitishaji vita wa wiki mbili huko Yemen hata hivyo nchi hiyo ilikiuka usitishaji vita huo katika masaa ya awali tu ya kuanza kutekelezwa.

Sambamba na kuenea maambukizi ya virusi vya corona duniani; Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amependekeza kuwa vita vyote na mapigano visitishwe duniani kote. Moja ya vita vibaya mno hii leo duniani ni vita vinavyoongozwa na muungano vamizi wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen ambavyo vimesababisha kutokea janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani. Kiasi kwamba hivi sasa raia wa Yemen wapatao milioni 22 kati ya jamii nzima ya nchi hiyo ya watu milioni 24 wanahitaji misaada ya kibinadamu. 

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN  

Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen inayoundwa na harakati ya Ansarullah na waitifaki wake imelipokea vizuri pendekezo hilo la Guterres. Serikali iliyojiuzulu ya Yemen na Saudia Arabia pia nazo zimeunga mkono pendekezo hilo. Turki al Maliki, msemaji wa muungano vamizi wa Saudia usiku wa kuamkia jana tarehe Tisa Aprili alitangaza habari hiyo ya kusitishwa vita huko Yemen na kueleza kuwa usitishaji vita huo utaendelea kwa muda wa wiki mbili; na baada ya hapo pia unaweza kuongezwa muda.  

Hii si mara ya kwanza kwa Saudi Arabia katika muda wa miaka mitano iliyopita kukaribisha utekelezaji wa usitishaji mapigano katika vita nchini Yemen. Mapatano yaliyofikiwa mwezi Disemba 2018 huko Stockholm chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa yalikuwa makubaliano ya mwisho ya usitishaji vita yaliyoafikiwa. Kwa mujibu wa mapatano hayo, ilielezwa kuwa usitishaji vita utekelezwe huko al Hudaydah ambako asilimia 70 ya bidhaa zinazoingia Yemen hutumia bandari hiyo. Pamoja na hayo lakini Riyadh haijaheshimu kivyovyote vile usitishaji vita huo na mara kwa mara unaendeleza mashambulizi dhidi ya mkoa wa al Hudaydah.  

Aidha vikosi vya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia umeshakiuka mapatano hayo kwa zaidi ya mara 55 elfu tangu usitishaji vita ulipoanza kutekelezwa mwezi Disemba mwaka 2018 katika mkoa wa al Hudaydah na kupelekea kuuliwa na kujeruhiwa  Wayemeni zaidi ya elfu tano. Televisheni ya al Masira ya Yemen imezinukuu duru za kijeshi za nchi hiyo na kutangaza kuwa muungano vamizi nchini humo unaoongozwa na Saudia mwezi Machi uliopita ulikiuka  usitishaji vita mara 4,428 mkoani al Hudaydah magharibi mwa Yemen. 

Hivi sasa pia huku Saudi Arabia ikisema kuwa imekubali kusitisha vita huko Yemen, Brigedia Jenerali  Yahya Saree Msemaji wa jeshi la Yemen amekadhibisha madai ya muungano huo vamizi unaaongozwa na Saudia kwamba umesimamisha mashambulizi huko Yemen na usitishaji umeanza kutekelezwa nchini humo na kusisitiza kuwa muungano huo umeyashambulia maeneo mbalimbali ya Yemen tangu kuanza kutangazwa usitishaji vita huo. Harakati ya Ansarullah ya Yemen pia imetangaza kuwa muungano huo vamizi umezisimamisha huko Djibouti meli 14 za Yemen  zilizokuwa zimepakia bidhaa za mafuta na 3 zenye bidhaa za chakula  licha ya kuwa na kibali cha kimataifa.   

Brigedia Jenerali, Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen  

Kwa msingi huo, inaonekana kuwa kutangaza usitishaji vita ni mbinu fulani tu ya Saudia ambayo huwenda ikapelekea kupungua mashambulizi hata hivyo haitapelekea kusitishwa mashambulizi dhidi ya Yemen. Katika mazingira haya ya sasa Saudi Arabia inahitajia mbinu hii kuliko wakati mwingine wowote. Ifahamike kuwa Riyadh iko chini ya mashinikizo makubwa katika vita dhidi ya Yemen kwa kuwa, mashinikizo hayo kabla ya jambo lolote, yanatokana na mafanikio ya kioperesheni ya jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen. Katika upande mwingine iwapo utawala wa Aal Saud usingeafiki pendekezo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kusitisha mapigano huko Yemen ungekuwa pia chini ya mashinikizo zaidi ya fikra za waliowengi na dhati yake ya kupenda vita ingelidhihirika zaidi. Utawala wa Aal Saud ndani ya Saudia pia unakabiliwa na maambukizi makubwa ya corona ambapo vyombo vya habari vimeripoti juu ya kuambukizwa virusi hivyo wana wafalme 15 wa Saudia na huku Mfalme Salman na Mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman wakihofia pakubwa kuambukizwa virusi vya corona.   

Inaonekana ni kwa sababu hiyo ndio maana Muhammad al Bakhiti Mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Harakati ya Ansarullah la Yemen akasisitiza kuwa Saudi Arabia haina mwamana, kwani imetangaza mara kadhaa kwamba inahitihimisha oparesheni za kijeshi huko Yemen lakini haitekelezi ahadi zake; na hatua ya hivi sasa ya ukoo wa Aal Saud ya kuunga mkono usitishaji vita itakuwa ni mbinu tu ambayo Riyadh inajaribu kuitumia ili kufidia hasara na maafa iliyopata  huko Yemen iwapo mzingiro dhidi ya Yemen hautasambaratishwa. 

Nukta ya mwisho ni kuwa usitishaji vita huko Yemen utategemea ni kiasi gani Saudia itahitimisha mzingiro wake wa pande zote dhidi ya nchi hiyo kwa sababu lengo la kusimamisha vita ni kusaidia kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona; na lengo hili haliwezi kufikiwa ndani ya kiza cha kuzingirwa kila pande Yemen.  

Tags

Maoni