Apr 10, 2020 11:59 UTC
  • Muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia waendelea kukiuka usitishaji vita nchini Yemen

Huku Martin Griffiths, Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen na Nayef Falah al Hajraf, Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi wakipongeza uamuzi wa kusitisha vita na mapigano nchini Yemen, muungano vamizi unaoongozwa na Saudia katika vita huko Yemen umeendelea kukiuka usitishaji vita huo.

Ukiukaji huo wa usitishaji vita, unaripotiwa masaa machache tu baada ya msemaji wa muungano vamizi wa Saudia Kanali Turki al-Malki kutangaza kuwa, usitishaji vita uliotangazwa na muungano huo utaendelea kwa muda wa majuma mawili na baada ya hapo inawezakana kuongeza muda wake.

Ripoti kutoka nchini Yemen zinaeleza kuwa, mashambulio ya mizinga yaliyofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia yamepelekea kwa akali watu wawili kuuawa kusini mwa mkoa wa al-Hudaydah magharibi mwa nchi hiyo.

Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen, ametangaza kuwa, licha ya kuweko tangazo la kusitisha vita lililotolewa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia, lakini vikosi vya muungano huo wa kijeshi vimeendelea kufanya mashambulio katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Shule iliyoharibiwa katika mashambulio ya Saudia na washirika wake dhidi ya Yemen

Kabla ya hapo viongozi mbalimbali wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen walikuwa wamelibeza tangazo la kusitisha vita la muungano wa kijeshi wa Saudia na kulitaja kama “mchezo wa mpya wa kisiasa wa Saudia na washirika wake”.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia.

Tags

Maoni