Apr 27, 2020 00:40 UTC
  • Msimamo mmoja wa dunia dhidi ya mpango wa utawala wa Kizayuni na uungaji mkono wa Marekani kwa mpango huo

Serikali ya Rais Donald Trump imekuwa ikichukua hatua zisizo za kawaida katika kuunga mkono utawala haramu wa Kizayuni ambapo kati ya hatua hizo ni kuafiki rasmi suala la kuunganishwa maeneo ya Ukingo wa Magharibi na maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo bandia.

Hatua hiyo ya Israel pamoja na uungaji mkono wa Washington, umekabiliwa na upinzani mkali wa jamii ya kimataifa. Katika uwanja huo, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Russia kama mshindani wa kimataifa wa Marekani, kwa pamoja zimekuwa na msimamo mmoja dhidi ya mpango wa Tel Aviv wa kuziunganisha baadhi ya ardhi za Ukingo wa Magharibi na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), mpango ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani. Nickolay Mladenov, Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Asia Magharibi, ameuelezea mpango huo wa utawala haramu wa Kizayuni kuwa ni tishio kwa usalama na amani ya eneo. Akiashiria makubaliano yaliyofikiwa kati ya Benjamin Netanyahu na Benny Gantz, ambao ni viongozi wa Likud na Blu na Nyeupe kwa ajili ya kuunda serikali ya mseto amebainisha kuwa viongozi hao wa Kizayuni wamekusudia kuziunganisha sehemu za Ukingo wa Magharibi na ardhi zingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (yaani Israel) kuanzia mwezi Julai 2020. Lengo lao ni kwamba kutokana na uungaji mkono wa kila upande wa Rais Donald Trump kwa utawala wa Kizayuni, na madamu serikali ya Washington ingali madarakani, hivyo ni lazima wahakikishe mpango huo unatekelezwa. Kuhusiana na suala hilo Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema: "Uamuzi kuhusiana na kuziunganisha ardhi za Ukingo wa Magharibi uko mikononi mwa Tel Aviv. Huo ni uamuzi wa Israel." Pamoja na hayo yote, hata washirika wa Ulaya wa Marekani pia wameonyesha kutoridhishwa na uamuzi huo wa utawala wa Kizayuni. Kuhusiana na suala hilo, Josep Borrell Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kuwa, EU haitambui rasmi umiliki wa Israel kwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Ukingo wa Magharibi.

Nickolay Mladenov, Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Asia Magharibi

Taarifa iliyotolewa na Borrell kuhusiana na suala hilo imesisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yakiwemo ya nambari 242 la mwaka 1967 na  nambari 338 la mwaka 1973 hautambui umiliki wa Israel wa ardhi za Ukingo wa Magharibi na kwamba uunganishwaji wowote wa ardhi hizo utachukuliwa kuwa ni kielelezo tosha cha ukiukaji wa sheria za kimataifa. Umoja wa Ulaya na nchi tofauti za Ulaya zikiwemo Ufaransa, Uingereza na Ujerumani, zimesisitiza pia kupinga mpango huo wa baraza la mawaziri la serikali ya umoja wa kitaifa la Israel chini ya uongozi wa Benjamin Netanyahu na Benny Gantz. Aidha Russia kama mmoja wa wanachama wa tume ya pande nne na mwenye nafasi muhimu katika uga wa Asia Magharibi, imepinga pia hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni. Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ametoa taarifa ambapo sambamba na kuonyesha wasi wasi wake juu ya siasa za utawala wa Kizayuni na mpango wake wa kuziunganisha sehemu ya ardhi za Ukingo wa Magharibi, amesema kuwa siasa hizo zitadhoofisha mwenendo wa utatuzi wa mgogoro wa Palestina. Msimamo mmoja wa dunia katika kupinga mpango unaokiuka sheria wa utawala haramu wa Kizayuni, ambao kimsingi ni wa pande tatu za wajumbe wa kamati ya pande nne yaani Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Russia, ni ishara nyingine ya kutengwa Marekani ambaye ni mjumbe mwingine wa kamati hiyo kutokana na uungaji mkono wake usio na masharti kwa utawala wa Kizayuni na pia kulaaniwa utawala huo bandia hasa kutokana na hatua zake zisizohalalishika na zilizo dhidi ya ubinaadamu dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina. Hivi sasa karibu asilimia 52 ya Ukingo wa Magharibi inadhibitiwa moja kwa moja na utawala wa Kizayuni. Mbali na vitongoji haramu 15 eneo la Quds Mashariki, mwishoni mwa mwaka jana utawala huo bandia ulianzisha  kinyume cha sheria zaidi ya vitongoji 150 na vituo vya upekuzi 128 katika Ukingo wa Magharibi na karibu Wazayuni laki sita na elfu 60 wanaishi katika vitongoji hivyo kinyume cha sheria na maazimio ya Baraza la Usalama.

Trump na Netanyahu wanaolaaniwa na kupingwa na jamii nzima ya kimataifa

Umoja wa Mataifa na nchi nyingi za dunia, zinaichukulia hatua ya utawala haramu wa Israel ya kuanzisha ujenzi wa vitongoji katika eneo la Ukingo wa Magharibi kuwa inakiuka sheria  za kimataifa kwa kuwa katika vita vya mwaka 1967 utawala huo ulilivamia eneo hilo na kwa mujibu wa maamuzi ya Geneva, ujenzi wowote wa utawala wa Kizayuni katika maeneo uliyoyavamia, hauruhusiwi. Aidha azimio nambari 242 la Umoja wa Mataifa pia linautaka utawala huo wa Kizayuni kuondoka katika ardhi ulizozikalia kwa mabavu mwaka 1967 ukiwemo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Pamoja na hayo Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala huo na chini ya uungaji mkono kamili wa Rais Trump wa Marekani sambamba na kuwasilisha mpango wa Muamala wa Karne, si tu kwamba hajasitisha ujenzi wa vitongoji, bali hivi sasa kwa kushirikiana na Benny Gantz, mshirika wake katika serikali ya umoja wa kitaifa, anakusudia kuyaunganisha maeneo ya Ukingo wa Magharibi na  ardhi zingine zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. Hii ni katika hali ambayo upinzani wa jamii ya kimataifa dhidi ya hatua hizo za utawala katili wa Kizayuni, umepelekea utawala huo kutengwa siku hadi siku sambamba na kulaaniwa hatua zake zilizo kinyume cha sheria na dhidi ya ubinaadamu. Kama ambavyo pia uungaji mkono wa serikali ya Trump kwa utawala huo khabithi, unaendelea kulaaniwa na jamii ya kimataifa.

Tags

Maoni