May 22, 2020 05:58 UTC
  • Mnong'ono wa kutokomea utawala ghasibu wa Israel wasikika katika mitaa ya Tel Aviv

Intifadha ya taifa la Palestina imevuka mipaka ya kijografia ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuingia katika hatua muhimu ambapo sasa mnong'ono wa kumalizika na kusambaratika utawala ghasibu wa Israel umeanza kusikika katika mitaa ya Tel Aviv.

Katika ujumbe alioutoa siku ya Jumatano kwa mnasaba wa kukaribia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds, Meja Jenerali Muhammad Baqiri, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa stratijia ya mapambano ya Palestina imeenea na kuzishirikisha nchi nyingi kiasi kwamba jambo hilo limewatia kiwewe na wasiwasi mkubwa maghasibu wa ardhi za Palestina.

Ni zaidi ya miaka 70 sasa ambapo wananchi madhulumu wa Palestina wamefukuzwa katika nyumba na ardhi zao na kulazimika kuishi kama wakimbizi katika mataifa mengine. Taifa hilo linaendelea kukabiliwa na njama mpya za kila mara za Marekani dhidi ya Waislamu na Wapalestina. Katika mwezi wa kwanza mtukufu wa Ramadhani baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini (MA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza juu ya msingi muhimu wa Mapinduzi ya Kiilamu wa kupambana na dhulma na kutangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Quds. Alitangaza siku hiyo kuwa Siku ya Quds ili kuifanya kuwa nembo ya kuimarishwa umoja na mshikamano wa umma wa Kiislamu na watu wengine wanaopigania uhuru wa mataifa, katika kuunga mkono taifa Palestina linalodhulumiwa na kukandamizwa na Wazayuni wa Israel. Suala hilo linathibitisha wazi kwamba mapambano dhidi ya madhalimu na kuwatetea wanyonge ni moja ya misingi muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na bila shaka taifa la Iran lina msimamo thabiti katika uwanja huo.

Wananchi wa Tanzania wakiandamana kuadhimisha Siku ya Quds

Alipokutana siku ya Jumanne na Hussein Abdullahiyan, Msaidizi Maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge), anayeshughulikia masuala ya kimataifa, Khalid Qaddumi, Mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS mjini Tehran alisifu na kushukuru hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na majlisi hiyo, ya kupasisha sheria ya kukabiliana na utawala haramu wa Israel. Alisema: Katika hali ambayo baadhi ya serikali zinachukua hatua za kuuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa nchi ya kwanza kuchukua hatua muhimu ya kupasisha sheria ya kukabiliana na hatua za kiuadui za utawala wa Kizayuni zinazohatarisha amani na usalama wa eneo.

Jatika miaka ya karibuni, walimwengu wamekuwa wakishuhudia matukio mbalimbali katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni jambo ambalo bila shaka linaonyesha mafanikio makubwa ya mrengo wa mapambano ya Kiislamu katika ardhi hizo na wakati huohuo kudhoofika na kukaribia kusambaratika utawala ghasibu wa Israel.

Akizungumzia suala hilo, Robert Fantina, mtafiti wa masuala ya haki za binadamu wa nchini Marekani ameandika makala akiufananisha utawala huo na ule wa kipindi cha ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na kusema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa utawala huo wa Kizayuni kusambaratika na kufikia mwisho wake kupitia kampeni za kiusanii, vyombo vya habari na vikwazo vya kiuchumi na kifedha dhidi ya utawala huo wa kibaguzi.

Robert Fantina, mtafiti na mtaalamu wa masuala ya haki za binadamu wa nchini Marekani

Ni wazi kwamba utawala huo unaoua watoto wadogo na kutekeleza jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina hauko tayari hata kidogo kutoa fursa wala kuwarejeshea watu hao haki zao ulizozipora. Njama kama vile za mpango wa Muamala wa Karne ambao ulibuniwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili ya kuunganisha Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel ni njama zinazolenga kukanyaga zaidi haki za Wapalestina, ili kuunusuru utawala huo na kuzuia usisambaratike.

Ujumbe wa Meja Jenerali Muhammad Baqeri, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds Tukufu unaashiria wazi nukta hiyo muhimu. Ujumbe huo unaashiria ukweli wa matukio yanayoendelea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuichukulia Intifadha ya Palestina kuwa harakati iliyoenea hadi nje ya mipaka ya Palestina, na ambayo imeingia katika hatua mpya na muhimu ya uhai wake. Amesisitiza jambo hilo kwa kusema: Sasa mnong'ono wa kutokomea utawala ghasibu wa Israel umeanza kusikika katika mitaa ya Tel Aviv.