May 22, 2020 08:02 UTC
  • Palestina yakataa misaada ya Imarati iliyotumwa kupitia Tel Aviv

Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekataa kupokea misaaada iliyotumwa nchini humo na Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia uwanja wa ndege wa Tel Aviv.

Katika kikao na waandishi wa habari jana Alkhamisi, Mai Kaila, Waziri wa Afya wa Palestina amesema taifa hilo limekataa kupokea misaada ya kitiba iliyotumwa na Imarati kupitia Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion ulioko katika mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, Tel Aviv.

Amesema UAE ilipuuza mashauriano na ushirikiano na Palestina juu ya kutumwa nchini humo dawa na vifaa vya kupambana na ugonjwa wa Covid-19 (Corona). Amefafanua kuwa, "sisi ni taifa lenye mamlaka ya kujitawala, walipaswa kuonyesha ushirikiano kwanza kabla ya kutuma shehena ya misaada."

Wapalestina wamesema kitendo hicho cha Umoja wa Falme za Kiarabu kuwatumia misaada kupitia Tel Aviv ni njama za kuficha mpango wa nchi hiyo ya Kiarabu wa kufanya wa kawaida uhusiano wake na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Baadhi ya nchi za Kiarabu kama Imarati zinafanya jitihada za kuboresha uhusiano na Israel

Siku ya Jumanne, ndege ya mizigo ya Etihad ya Imarati iliyokuwa imesheheni misaada ya kitiba kwa ajili ya wananchi wa Palestina ilitua katika Uwanja wa Ndege wa  Ben Gurion ulioko katika mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, Tel Aviv, ikitokea Abu Dhabi.

Hii ni mara ya kwanza kwa ndege ya UAE kutua wazi wazi Israel, licha ya kuwa nchi hiyo haina uhusiano wowote rasmi na utawala huo pandikizi unaokaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

 

Tags

Maoni