May 22, 2020 11:17 UTC
  • HAMAS: Jenerali Esmail Qaani anafuata nyayo zile zile za Qassem Soleimani katika kuitetea Palestina

Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Palestina HAMAS amesisitiza kwamba msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na Palestina ungali thabiti na imara.

Saleh al-Arouri, amesisitiza kwamba Jenerali Esmail Qaani Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC anafuata njia na nyendo zile zile za shahidi Qassem Soleimani katika kuliunga mkono taifa la Palestina. Akibainisha kwamba shahidi Haji Qassem Soleimani aliyekuwa kamanda wa kikosi cha Quds daima alikuwa mkweli, shujaa na muungaji mkono mkubwa wa muqawama, al Arouri ameongeza kwamba shahidi huyo hakupinga jambo lolote linalohusu muqawama na uungaji mkono kwa muqawama huo. Kadhalika Saleh al-Arouri ameubebesha utawala wa Kizayuni dhima ya mzingiro dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza na kusisitiza kwamba, utawala bandia wa Israel unafanya njama za kuibua mpasuko ndani ya Palestina na ndani ya nchi za Kiarabu ili pande hizo zishadidishe mashinikizo dhidi ya eneo la Gaza.

Esmail Qaani Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC

Naye kwa upande wake Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islam ya Palestina sambamba na kusisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuzembea hata kidogo katika kuunga mkono muqawama amesema kuwa, hii leo muqawama katika eneo la Asia Magharibi ni wenye nguvu kuliko wakati mwingine wowote ule. Ziyad al-Nakhalah ameashiria pia misaada na uungaji mkono wa Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kiongozi wa zamani wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC kwa muqawama wa eneo na kubainisha kwamba shahidi Soleimani alikuwa mwakilishi wa Iran katika kuunga mkono muqawama na kwamba kifo chake kimezidisha azma ya kuendeleza uungaji mkono kwa muqawama.