May 22, 2020 12:31 UTC
  • Jeshi la Lebanon: Kukombolewa kusini mwa Lebanon yalikuwa mafanikio makubwa dhidi ya Israel

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Lebanon amehutubu kwa mnasaba wa mwaka wa 20 wa kukombolewa eneo la kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu na kuongeza kwamba, lau kama si kusimama imara kwa taifa hilo, basi mafanikio hayo makubwa yasingepatikana.

Joseph Aoun ameyasema hayo kwa mnasaba wa mwaka wa 20 wa ukombozi wa maeneo ya kusini mwa Lebanon na kusisitiza kuwa, 'Idi ya Muqawama na Ukombozi' ni mafanikio makubwa kwa historia ya Lebanon dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni. Kamanda Mkuu wa Jeshi la Lebanon ameongeza kwamba taifa la Lebanon litaendelea kusimama imara katika kutetea haki yake na kukamilisha mafanikio ya kurejesha udhibiti wa maeneo ya Mashamba ya Shebaa, miinuko ya Kafru Shiba na sehemu ya kaskazini mwa kijiji cha Ghajr pamoja na kuzima njama za adui Mzayuni. Aidha Joseph Aoun amevitaka vikosi vya Lebanon kuwa macho na utayari zaidi na kujitolea katika njia ya kuitumikia nchi.

Shahidi Luteni Jenerali Qassem alikuwa mstari wa mbele katika kuwafurusha Wazayuni kutoka maeneo ya kusini mwa Lebanon

Wakati huo huo Sheikh Nabil Qauq, Mjumbe wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Hibullah ya Lebanon sambamba na kupongeza nafasi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC katika kukombolewa maeneo ya kusini mwa Lebanon mwaka 2000, amesema kuwa baada ya kukombolewa maeneo hayo,  kamanda huyo bila kusubiria shukrani wala kusifiwa na yeyote kwa hilo, aliutoa muqawama katika kipindi cha kushindwa na kuungiza katika kipindi cha ushindi. Itakumbukwa kuwa baada ya miaka 18 ya muqawama wa raia wa Lebanon, hatimaye tarehe 25 Mei 2020 utawala haramu wa Kizayuni ulilazimika kuondoka kwa madhila kutoka maeneo ya kusini mwa nchi hiyo. Kufuatia hali hiyo siku hiyo ilipewa jina la 'Idi ya Muqawama na Ukombozi.'

Tags

Maoni