May 23, 2020 02:36 UTC
  • Jihadul Islami: Iran inahimili vikwazo vya kila namna kwa ajili ya kuihami Palestina

Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amegusia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds yaliyofanyika jana Ijumaa kote duniani na kukumbusha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejikubalisha kuhimili na kuvumilia mashinikizo na vikwazo vya kila namna vya mabeberu kwa ajili ya kuhami malengo matukufu ya Palestina.

Nafiz Izam alisema hayo jana na kuongeza kuwa, ujumbe wa Siku ya Kimataifa ya Quds ni kuwatangazia watu wote duniani kwamba malengo matukufu ya Palestina yako hai mbele ya umma wa Kiislamu na kamwe hayawezi kufa.

Amesema, licha ya kuweko njama nyingi sana za kuangamiza malengo matukufu ya Palesina, lakini katika Siku ya Quds, Waislamu kote ulimwenguni huwatangazia walimwengu wote kwamba wameshikamana vilivyo na Kibla chao cha Kwanza yaani Msikiti wa al Aqsa na mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas na malengo yote matukufu ya Palestina.

Nembo ya harakati ya Jihadul Islami ya Palestina

 

Mjumbe huyo mwandamizi wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina vile vile amegusia jinsi Wazayuni wanavyofanya njama za kufuta kabisa athari za Kiislamu katika mji wa Quds na kusema, Quds ndio mhimili wa mapambano kwani Wazayuni hawajasita hata mara moja kufanya njama za kuuyahudisha mji huo mtukufu, kuwafukuza wenyeji wake, kuwabana Waislamu na kuwapora mali na ardhi zao. Hata hivyo amesema, njama na ukatili wote huo umefeli kwani Quds imekita mizizi katika nyoyo za Wapalestina na kwenye nyoyo za wananchi wa nchi za Kiarabu na wa ulimwengu mzima wa Kiislamu.

Miongo minne iliyopita, Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds. Mwaka huu siku hiyo muhimu iliadhimishwa jana Ijumaa tarehe 22 Mei 2020 kote ulimwenguni. 

Tags

Maoni