May 23, 2020 02:37 UTC
  • Chama cha al Ghad Tunisia: Kambi ya muqawama ishirikiane vilivyo kukabiliana na Wazayuni

Katibu Mkuu wa chama cha al Ghad cha Tunisia amesisitiza kuwa, ni jambo la dharura sana kuimarishwa kambi ya muqawama kadiri inavyowezekana katika kukabiliana na Wazayuni maghasibu.

Katibu Mkuu wa chama hicho jana Ijumaa aliliambia Shirika la Habari la IRNA kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kupongezwa na kushukuriwa sana kwa uungaji mkono wake mkubwa kwa malengo matukufu ya Palestina na kusisitiza kuwa, kilichoifanya Siku ya Kimataifa ya Quds kuwa harakati kubwa dhidi ya Uzayuni leo hii ni uungaji mkono wa kipekee wa wananchi kwa siku hiyo ambayo leo inaadhimishwa kwa hamasa kubwa dunia nzima.

Katibu Mkuu wa chama cha al Ghad cha Tunisia ameongeza kuwa, Siku ya Kimataifa ya Quds sasa hivi imekuwa ni harakati ya kimataifa ya kupambana na Uzayuni na inazidi kufichua muundo wa kijinai na kikatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Harakati mbalimbali za muqawama katika ulimwengu wa Kiislamu zimesimama imara kupigania haki

 

Siku ya Quds ni dhihirisho la umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu hususan katika taifa la Waislamu la Iran kwani nchini Iran, suala la Palestina uungaji mkono kwa malengo ya Quds Tukufu ni suala la kwanza kabisa duniani.

Itakumbukwa kuwa, miongo minne iliyopita, Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds. Mwaka huu siku hiyo muhimu iliadhimishwa jana Ijumaa tarehe 22 Mei 2020. Maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika zaidi mitandaoni kutokana na marufuku ya kukusanyika watu iliyosababishwa na ugonjwa wa corona.

Tags

Maoni