May 23, 2020 03:35 UTC
  • Sayyid Nasrallah: Bila shaka Israel itasambaratika; vita asili vitakuwa na Marekani

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema hakuna shaka kuwa utawala wa Israel utasambaratika na amesisitiza kuwa, vita asili vitakuwa na Marekani.

Sayyid Hassan Nasrallah Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon aliyasema hayo jana Ijumaa  mjini Beirut katika hotuba kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds na kusisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni ni utawala uliopo kinyume cha sheria, ni utawala ambao ni kashfa ya ufisadi, ni utawala ghasibu, vamizi na ni donda la saratani ambalo lazima liangamizwe. Ameongeza kuwa, Palestina kutoka ‘Bahari hadi Mto’ ni milki ya Wapalestina na hivyo warejeshewe ardhi hiyo yote.

Sayyid Nasrallah ameendelea kubaini kuwa, njia ya ukombozi wa Palestina ni muqawama na mapambano ya kutumia silaha na ameongeza kuwa, pamoja na dosari zake zote, mapambano ndio njia pekee ya kukomboa ardhi za Palestina na matukufu yake na hivyo njia zingine zote ghairi ya hii ni kupoteza wakati tu.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameendelea kusema kuwa, vita vya ukombozi ni vita vya muda mrefu na vitachukua muda mwingi na kuongeza kuwa, watu wa Palestina kidhahiri wanapigana na Israel lakini katika batini vita hivyo ni makabiliano na Marekani.

Mji wa Quds (Jerusalem) ambao unakaliwa kwa mabavu na Israel

Sayyid Nasrallah amesema vita ambavyo vimejiri Asia Magharibi katika miongo ya hivi karibuni ikiwa ni pamoja na hujuma ya Saddam, dikteta  aliyetimuliwa wa utawala wa Baath wa Iraq dhidi ya Iran na pia vita vya hivi sasa vya Saudia dhidi ya Yemen, vyote ni kwa lengo la kulinda mlingano wa nguvu kwa maslahi ya Israel. Amesisitiza kuwa  lengo la vita hivyo si kingine isipokuwa ni kuulinda utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kiongozi wa Hizbullah ameashiria nafasi ya Iran katika mhimili wa muqawama na mlingano wa makabiliano na Israel na kusema leo Iran inalengwa na kukabiliwa na vitisho na uhasama wa Marekani kwa sababu inaongoza mhimili wa muqawama.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kuwa, mhimili wa muqawama utaendelea kusimama kidete na kwamba mpango wa kuimarisha nguvu za mhimili wa muqawama utaendelea. Aidha amesisitiza kuwa uadui wa Israel hauwezi kusimamisha mhimili wa muqawama nchini Iran au katika nchi zingine kama vile Yemen, Syria, Lebanon na Iraq.

Sayyid Hassan Nasrallah amelaani vikali hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema mkondo huu utafeli na ni uhaini.

 

Tags

Maoni