May 24, 2020 02:45 UTC
  • Vipengee vitatu vikuu vya hotuba ya Siku ya Quds ya Sayyid Hasan Nasrullah kuhusu Palestina

Sayyid Hasan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon siku ya Ijumaa alitoa hotuba muhimu kwa mnasaba wa mwaka wa 41 wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds na sisi katika uchambuzi huu wa kisiasa tutachambua baadhi ya vipengee muhimu vya hotuba yake hiyo.

Kipengee cha kwanza kabisa cha hotuba ya Sayyid Nasrullah, kilikuwa ni kutilia mkazo suala la kulindwa jiografia ya Palestina kutoka "Baharini hadi Mtoni." Bendera ya utawala wa Kizayuni ina rangi mbili buluu juu na chini; jambo ambalo linaakisia kaulimbiu ya "Israel Kubwa" au ardhi kamili ya Israel ambapo kwa madai yao Wazayuni ardhi hiyo inaanzia Mto Nile hadi Mto Furat. Katika mkabala wa mtazamo huo baadhi ya viongozi wa kambi ya muqawama hususan Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na pia Sayyid Hasan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, wanatoa kaulimbiu nyingine kuhusu eneo la Palestina, kaulimbiu hiyo ni kutoka "Baharini hadi Mtoni." Kwa mtazamo wa viongozi hao wa kambi ya muqawama, utawala wa Kizayuni si tu unapaswa kusahau ndoto yake ya ardhi eti iliyoahidiwa inayotokea Mto Nile hadi Mto Furati, lakini hata katika hali iliyo nayo hivi sasa Israel, pia haistahamiliki, bali inabidi ardhi zote za Palestina zikombolewe; na utawala wa Kizayuni ufurushwe kikamilifu katika ardhi zote unazozikalia kwa mabavu. Hotuba hiyo ya Sayyid Hasan Nasrullah haikulaani tu uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa kupora na kuteka ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, bali imetoa majibu ya wazi ya kupinga kikamilifu mpango wa kibaguzi wa "Muamala wa Karne."

Quds ni yetu

 

Kipengee cha pili muhimu katika hotuba ya siku ya Ijumaa ya Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ni pale aliposema kuwa utawala wa Kizayuni ni dhaifu sana tofauti na unavyojigamba. Sayyid Nasrullah alisema: Tukiangalia kijuu juu tutaona kama vile wananchi wa Palestina wanapambana na Israel tu, lakini uhakika ni kwamba, vita hivyo ni vya kupambana na Marekani. Kwa maneno mengine ni kuwa, kama si uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni, basi Israel haina ubavu hata wa kujilinda. Hata Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alitumia lugha kama hiyo katika hotuba yake ya Ijumaa ya Siku ya Kimataifa ya Quds. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema: "Mhalifu mkuu wa janga la kutekwa na kukaliwa kwa mabavu Palestina ni tawala za nchi za Magharibi na siasa zao kishetani." Kwa upande wake, Sayyid Hasan Nasrullah yeye, hata anaamini kwamba mapigano ya miongo kadhaa ya hivi karibuni katika eneo hili vikiwemo vita vilivyoanzishwa na Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran na pia vita vilivyoanzishwa hivi sasa na Saudi Arabia nchini Yemen vimepangwa na kusimamiwa na Marekani kwa lengo la kulinda mlingano wa nguvu kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kipengee cha tatu kikuu kilichokuwemo kwenye hotuba ya "Sayyid wa Muqawama" ni pale aliposisitizia wajibu wa kupambana na utawala wa Kizayuni kwa kutumia silaha. Katika siku za hivi karibuni, viongozi wote wa kambi ya muqawama wamekuwa wakisisitiza kuwa, muqawama wa kutumia silaha ndiyo njia pekee ya kuikomboa Palestina. Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon naye alisisitiza katika hotuba yake ya jana ya Siku ya Kimataifa ya Quds kuwa, hiyo ndiyo njia pekee ya kuzikomboa ardhi za Palesitna na matukufu yake na kwamba njia nyingine zote zisizokuwa hiyo ni kupoteza wakati. Hivyo, kutumia silaha na kupinga mazungumzo na utawala wa Kizayuni ni kipengee cha tatu muhimu kilichosisitizwa na Sayyid Hasan Nasrullah katika hotuba yake ya Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo ni Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mtukufu wa Ramadhani.

 

Kiujumla ni kwamba kambi ya muqawama imepata mafanikio makubwa katika kupambana na utawala wa Kizayuni na madola ya kibeberu. Wakati ambapo wale waliokuwa na tamaa ya kupata chochote kupitia mapatano na mazungumzo na utawala wa Kizayuni, wanazidi kukata tamaa hasa baada ya kupigwa rungu la "Muamala wa Karne" kutoka kwa Marekani; muamala ambao lengo lake hasa ni kuiangamiza kikamilifu kadhia ya Palestina. Kiujumla ni kwamba hotuba ya Sayyid Hasan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon imeashiria kwamba, muqawama wa kutumia silaha ndiyo njia fupi zaidi ya kuikomboa Palestina. Hii ni kusema kuwa hata hatua ya Marekani ya kuiwekea Iran mashinikizo na vikwazo vya kila namna ni kutokana na uhakika kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiye muungaji mkono mkuu wa muqawama wa kutumia silaha kukabiliana na utawala pandikizi wa Israel. 

Tags

Maoni