May 24, 2020 07:09 UTC
  • Onyo la Russia kuhusu madhara ya hatua za Wazayuni dhidi ya Palestina

Hatua zilizo kinyume cha sheria na zisizo za kibinadamu za Israel dhidi ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina zimepamba moto sana katika miaka ya hivi karibuni. Mbali na kuwaua Wapalestina hasa katika Ukanda wa Ghaza, utawala wa Kizayuni umeongeza sana kasi ya kupora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Sasa hivi utawala wa Kizayuni unajiandaa kupora ardhi zaidi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina na kuziingiza katika ardhi nyingine za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu tangu mwaka 1948. Vitendo hivyo vinalaaniwa kote duniani na katika hatua ya karibuni kabisa Russia imeionya Israel kuhusu madhara ya kuteka ardhi zaidi za Wapalestina. 

Katika tamko lake hilo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema, hatua ya Israel ya kuamua kupora ardhi mpya za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan itachochea machafuko mapya Asia Magharibi. Kwa mujibu wa tamko hilo, hatua za Israel za kupora ardhi zaidi za Wapalstina itazusha mapigano na machafuko ndani ya Palestina na ni tishio kwa usalama wa eneo hilo zima. Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeongeza kuwa, Moscow inaitahadharisha Israel kwa kutoheshimu kwake makubaliano ya kimataifa ya kupunguza hali ya wasiwasi na machafuko kwenye eneo la Asia Magharibi. Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia naye alisema siku ya Jumatano usiku wakati alipozungumza na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Gabi Ashkenazi kwamba, Russia inapinga vikali mpango wa utawala wa Kizayuni wa kupora ardhi zaidi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.  Kwa kweli Moscow inaamini kuwa, hatua hiyo ya Israel haina lengo jingine isipokuwa kushadidisha hali ya wasiwasi na mapigano huko Palestina na pia kuzidi kuhatarisha usalama wa eneo la Asia Magharibi ambalo hata hivi sasa halina utulivu kutokana na utawala wa Kizayuni kufanya jinai za mara kwa mara dhidi ya wananchi kama wa Syria na kutoheshimu hata kidogo haki ya kujitawala taifa la Lebanon. 

 

Utawala wa Kizayuni umekusudia kupora ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan  ifikapo mwezi Julai mwaka huu. Hivi sasa karibu asilimia 52 ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan inakaliwa kwa mabavu moja kwa moja na utawala wa Kizayuni. Mbali na vitongoji 15 vya Kizayuni vilivyojengwa kinyume cha sheria huko Baytul Muqaddas Mashariki, mwishoni mwa mwaka jana yaani 2019, kulijengwa zaidi ya vitongoji 150 vya Kizayuni na vituo 128 vya polisi Wazayuni. Mwaka huo pia walowezi laki sita na 70 elfu wa Kizayuni walipewa makazi kwenye vitongoji hivyo haramu. 

Mpango mpya wa Israel wa kupora ardhi zaidi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan mwezi Julai mwaka huu, unaungwa mkono kikamilifu na serikali ya Donald Trump ya Marekani. Katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu wa 2020 kwenye Ikulu ya Marekani, White House, Trump alizindua mpango wake wa "Muamala wa Karne" akiwa pamoja na Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, akidai kuwa eti kwa njia hiyo ndipo itawezekana kumaliza kabisa mzozo baina ya Wapalestina na Wazayuni. Kimsingi mpango huo umekusudia kuiangamiza kikamilifu kadhia ya Palestina. Miongoni mwa vipengee vya mpango huo ni kukabidhiwa Wazayuni mji mtakatifu wa Quds ambao una Kibla cha Kwanza cha Waislamu na ndio mji mkuu wa daima wa nchi ya Palestina. Vile vile mpango huo umependekeza Israel ipore kwa uchache asilimia 30 nyingine ya ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Jinai za utawala wa Kizayuni hazina kifani

 

Lakini mpango huo wa "Muamala wa Karne" unapingwa na Wapalestina wa mirengo na matabaka yote. Hata viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambao walikuwa na tamaa ya kufanikiwa mazungumzo yao ya mapatano na Wazayuni, nao wamekata tamaa na wanaupinga vikali mpango huo. Saeb Erekat, Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO mapema jana Ijumaa alitangaza kumalizika ushirikiano wa kiusalama kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni. Kiujumla ni kwamba dunia nzima inapinga mpango huo wa kidhulma wa Marekani, lakini kama wanavyosisitiza wanamapambano wa Palestina; Israel na Wazayuni wengine wote hawaelewi lugha yoyote isipokuwa mapambano ya silaha. Hivyo njia pekee ya kuweza kukomboa ardhi za Palestina ni muqawama wa kutumia silaha.

Tags

Maoni