May 24, 2020 09:42 UTC
  • Ansarullah yafichua nafasi ya Israel na US katika mashambulizi dhidi ya Yemen

Katibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ya nchini Yemen amesema Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ni washirika wa muungano vamizi wa kijeshi unaofanya mashambulizi dhidi ya wananchi wa Yemen.

Abdul‑Malik Badreddin al‑Houthi alisema haya jana jioni katika ujumbe aliotoa mwa mnasaba wa sikukuu ya Idul-Fitri inayoadhimishwa hii leo kote duniani na kusisitiza kuwa, taifa la Yemen litakabiliana na uvamizi huo kwa nguvu zake zote.

Katika ujumbe wake huo, al-Houthi amesema mashambulizi ya kila uchao yanayofanywa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia yanafanyika chini ya usimamizi na uangalizi wa utawala wa Washington na kwa ushirikiano kamili na utawala haramu wa Israel.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amewataka wananchi wa Yemen kuwaunga mkono kwa hali na mali wanamapambano walio katika mstari wa mbele kukabiliana na uvamizi huo wa Saudia na waitifaki wake katika eneo, na kwa uungaji mkono na baraka za Marekani na Israel.

Riyadh na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao katika hujuma zao dhidi ya Yemen, huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu

Haya yanaarifiwa huku duru za habari zikiarifu kuwa, ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudia zimeendelea kushambulia maeneo ya Yemen licha ya kutangaza usitishwaji vita wa muda.

Muungano vamizi wa Saudia mnamo Aprili 9 ulitangaza kuwa utasitisha kwa muda vita dhidi ya Yemen kwa lengo la kusaidia jitihada za kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 katika nchi hiyo. Hata hivyo masaa machache tu baada ya tangazo hilo, muungano huo ulitekeleza mashambulizi kadhaa dhidi ya Yemen. 

Tags

Maoni