May 25, 2020 03:55 UTC
  • Madai ya Marekani kuhusu serikali ya Pakistan kuyapa hifadhi makundi yanayopinga serikali ya Afghanistan

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imetoa ripoti na kudai kwamba serikali ya Pakistan sambamba na kuyapa hifadhi makundi yanayoipinga serikali ya Afghanistan, pia inayaunga mkono.

Ripoti hiyo ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) inasema, uwepo wa makundi yanayoipinga serikali ya Rais Ashraf Ghani nchini Pakistan, ni tishio kwa usalama na uthabiti wa Afghanistan. Hii ni katika hali ambayo Pakistan imepinga mara chungu nzima madai hayo ya Marekani na kwamba yanatolewa kwa lengo la kuzipotosha fikra za walio wengi na kujaribu kuhalalisha kufeli mipango ya Washington katika eneo. Kitendo cha kuituhumu Pakistan kwamba inayaunga mkono na kuyapa hifadhi makundi ya upinzani ya Afghanistan, ni stratijia ambayo imekuwa ikifuatiliwa kwa miaka mingi katika siasa za kigeni za Washington. Marekani kutoa tuhuma tofauti dhidi ya serikali ya Islamabad ikiwemo ya uwepo wa makundi yanayoipinga serikali ya Afghanistan ndani ya taifa hilo jirani, ni miongoni mwa mambo yaliyoshadidisha mzozo katika uhusiano ya Marekani na Pakistan katika miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo mzozo katika uhusiano wa nchi mbili ulishtadi zaidi baada ya kuingia madarakani serikali ya Rais Donald Trump ambaye amechukua mkondo wa siasa kali dhidi ya Pakistan hususan kupitia vitisho vya kuikatia misaada ya kifedha na kijeshi. Kwa mtazamo wa viongozi wa Islamabad, tuhuma za serikali ya Marekani dhidi ya Pakistan, hazina msingi wowote na kwamba nchi hiyo katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, imekuwa muhanga wa vita vya White House nchini Afghanistan.

Kuibua mvutano kati ya Pakistan na Afghanistan ndilo lengo kuu la Marekani

Aidha kwa mujibu wa viongozi wa Pakistan, baada ya uvamizi wa kijeshi wa Marekani na washirika wake katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) hapo mwaka 2001, hadi sasa Pakistan imeingia hasara ya zaidi ya dola bilioni 80. Kadhalika wanaamini kwamba sababu ya kushadidi machafuko na mashambulizi ya kigaidi nchini humo inatokana na hatua ya Washington ya kutaka kuendelea kuwepo kijeshi nchini Afghanistan. Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imeituhumu tena Pakistan kuwa inayapa hifadhi makundi yanayobeba silaha na yanayoipinga serikali ya Afghanistan wakati ambao White House imefeli katika makubaliano ya amani iliyotiliana saini na kundi la Taleban hapo tarehe 29 Fabruari mwaka huu mjini Doha, Qatar. Hapa unabainika wazi mtazamo huu kwamba lengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani kukariri tuhuma zilizopitwa na wakati dhidi ya serikali ya Islamabad, ni kujaribu kuzipotosha fikra za walio wengi katika eneo kuhusu kufeli mipango yake baada ya kutiliana saini makubaliano ya amani na kundi la Taleban nchini Qatar. Suala ambalo pia limehatarisha hata mazungumzo kati ya Waafghani ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika mara baada ya kutiwa saini makubaliano hayo ya mjini Doha.

Marekani iliyofeli Afghanistan inatoa tuhuma tofauti zisizo na msingi kujaribu kufunika kufeli kwake nchini humo

Pakistan imeweka bayana mara nyingi kwamba, madai ya kuunga mkono ugaidi ndani ya Afghanistan au kuyapa hifadhi makundi yanayoipinga serikali ya nchi hiyo mbali na kuwa na taathira hasi kwenye uthabiti na usalama wake yenyewe ambayo nayo inakabiliwa na wimbi la makundi ya kufurutu ada, kimsingi hayana mantiki kwa kuwa hatua kama hiyo itakuwa na matokeo mabaya kwenye usalama wa ndani wa nchi hiyo. Hata hivyo ni lazima ieleweke kwamba mbali na Marekani kujaribu kuituhumu Pakistan kuhusu uungaji mkono kwa vitendo vya ukatili na ugaidi nchini Afghanistan na kuchafua sura ya Islamabad kieneo na kimataifa, inakusudia pia kupitia tuhuma hizo iweze kushadidisha mzozo kati ya serikali ya Kabul na Islamabad. Hii ni kusema kuwa, uwepo wa tofauti na mizozo kati ya nchi hizo na pia njama za Marekani za kuidhihirisha Pakistan kuwa ni nchi hatari, kunaiandalia Washington uwanja wa kuendelea kubakia kijeshi nchini Afghanistan kwa kisingizio cha kukabiliana na hatari tarajiwa kutoka Pakistan. Hii ni katika hali ambayo kudhaminiwa usalama wa eneo hilo kunahitajia ushirikiano wa nchi mbili na bila shaka uingiliaji wa pande za kigeni hauwezi kuwa na matokeo mengine ghairi ya kushadidisha machafuko na ghasia katika eneo hilo.

Tags

Maoni