May 25, 2020 06:26 UTC
  • Israel yawashambulia wasimamishaji swala wa Palestina katika mwaka wa 53 wa kutekwa Masjidul Aqsa

Wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel wamewashambulia waumini wa Palestina na kuwazuia kusimamisha swala ya Idul Fitr katika Msikiti wa al-Aqsa.

Sambamba na kumalizika funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuwadia sikukuu ya Idul Fitr hapo jana Jumapili, Wapalestina walifika katika Msikiti wa al-Aqsa kwa ajili ya kusimamisha swala ya Idi lakini wakakabiliwa na shambulio la kinyama la askari wa utawala wa Kizayuni waliowazuia kuingia ndani ya msikityi huo. Hivyo swala hiyo muhimu iliswaliwa tu na wahudumu wa msikiti huo bila ya kushirikishwa watu wengine kutoka nje. Askari wa Kizayuni waliokuwa nje ya msikiti huo waliwashambulia waumini waliokuwa wamefika hapo kwa ajili ya kutekeleza ibada hiyo na kujeruhi makumi kati yao.

Kisingizio kilichotumiwa na askari hao kuzuia waumini kuingia ndani ya msikiti huo mtakatifu kwa ajili ya kusimamisha swala ya Idul Fitr ni kuwa milango ya msikiti huo imefungwa tokea miezi miwili iliyopita kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona. Pamona na hayo ukweli wa mambo ni kuwa askari hao wa utawala ghasibu wa Israel wamewazuia waumini wa Kipalestina kuingia na kuswali katika msikiti huo kutokana na umuhimu mkubwa ulionao msikiti huo kwa Waislamu.

Msikiti Mtakatifu wa al-Aqsa

Msikiti wa al-Aqsa ni Kibla cha kwanza cha Waislamu ambao huuita kwa jina la 'Haram Sharif.'

Mbali na hayo Msikiti wa al-Qsa ni nembo ya utambulisho wa kidini wa Wapalestina na vilevile ni nembo ya kughusubiwa na utawala haramu wa Israel ambao tokea mwaka 1967 hadi leo, yaani kwa muda wa miaka 53 umeuteka msikiti huo na kuwawekea vizuizi chungu nzima Waislamu wanaotaka kuingia katika msikiti huo kwa ajili ya kutekeleza ibada.

Juni 1967 vita vya siku 6 vilipiganwa kati ya Israel na nchi za Kiarabu, ambapo utawala huo haramu uliuteka Msikiti wa al-Qsa, na tokea wakati huo hadi sasa umekuwa ukifanya njama na juhudi kubwa za kubadilisha muundo wa kijamii wa eneo hilo na kuufanya kuwa wa Kiyahuhi. Hivi karibuni pia kufuatia mpango wa kibaguzi uliowasilishwa na Rais Donald Trump wa Marekani, mji mtukufu wa Quds (Jerusalem), sehemu uliko msikiti huo, umetajwa kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Isreal.

Jamamosi tarehe 23 mwezi huu wa Mei, Ofisi ya Kitaifa ya Kutetea Ardhi na Mapambano dhidi ya Ujenzi wa Vitongoji', na katika kuwadia mwaka wa 53 wa kutekwa Quds, ilitoa ripoti ikisema: 'Utawala wa Kizayuni unagali unaendeleza juhudi za kukalia kwa mabavu ardhi zilizobaki katika mji huu na hii ni katika hali ambayo wakazi Waislamu wa Baitul Muqaddas wanaendelea kukabiliwa na hali ngumu ya maisha. Mbali na hayo siasa zote za zamani za kubomoa na kuharibu nyumba za wakazi wa Baitul Muqaddas na 'usafishaji taratibu wa kibaguzi' kwa lengo la kubadilisha muonekano wa mji na kuuyahudisha taratibu, bado zinaendelea kutekelezwa.'

Waislamu wakiswali katika uwanja wa Masjidul Aqsa

Licha ya kuwa hivi sasa utawala wa Kizayuni unatumia kisingizio cha kuzuia maambukizi ya virusi vya corona kuwabana Wapalestina wasiingie katika Msikiti wa al-Aqsa lakini ni wazi kuwa utawala huo ulianza kutekeleza siasa hizo miaka mingi iliyopita na kwa kutumia mbinu tofauti. Mbinu hizo ni pamoja na kujenga uzio wa kibaguzi mwaka 2000, kuweka mipaka ya kiumri, kuanzisha vituo vya upekuzi kati ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na mji wa Baitul Muqaddas na vilevile kutundika mitambo ya ujasusi na usalama katika mji huo.

Mbali na kuwa hatua hizo za utawala ghasibu wa Israel zinakiuka moja kwa moja haki na uhuru wa kuabudu wa Waislamu wa Palestina, lakini ni wazi kuwa lengo lake kuu ni kutekeleza siasa za kuuyahudisha mji wa Quds. Licha ya kuwa mji wa Baitul Muqaddas ni eneo takatifu kwa Wapalestina, lakini wakati huohuo ni nembo ya utambulisho wao, kwa kadiri kwamba Intifadha yao ya Disemba 28 2000 ilianza kutokana na kuvunjiwa heshima Msikiti wa al-Aqsa. Bila shaka hujuma na mashambulio ya mara kwa mara yanayofanywa na askari wa utawala haramu wa Israel dhidi ya Waislamu wa Palestiana hayatawazuia wala kuwaogopesha kufika katika msikiti huo kwa ajili ya kutekeleza ibada zao kama ambavyo wamekuwa wakifanya tokea zama za kale.

Tags

Maoni