May 31, 2020 08:06 UTC
  • Mgogoro wa Palestina, Israel yakaribia kutumbukia katika vita au Intifadha mpya

Kuendelea uvamizi na sera za mabavu za Israel kumezidisha machafuko baina ya utawala huo ghasibu na raia wa Palestina kiasi kwamba, utawala huo haramu umeua shahidi Wapalestina wasiopungua wawili katika siku mbili zilizopita.

Wanajeshi wa Israel jana Jumamosi wamemuua kwa kumpiga risasi kijana mmoja wa Kipalestina katika mji mtakatifu wa Quds. Kijana mwingine wa Kipalestina aliuawa jana kwa kupigwa risasi na askari usalama wa Israel karibu na kitongoji cha Halamish huko kaskazini magharibi mwa Ramallah.

Sababu ya kuongezeka machafuko hayo ni harakati za utawala wa Kizayuni katika fremu ya utekelezaji wa mpango habithi wa Muamala wa Karne uliobuniwa na Rais Donald Trump wa Marekani. Trump alizindua rasmi mpango huo tarehe 28 Januari mwaka huu ambapo kwa mujibu wake, Wapalestina watapewa asilimia 15 tu ya ardhi yote ya Palestina na maeneo mengine karibu yote yanayozusha hitilafu au yale yaliyovamiwa na kukaliwa kwa mabavu ya Ukingo wa Magharibi yatachukuliwa na utawala haramu wa Israel. 

Intifadha mpya

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi wa utawala huo Benny Gantz wamekubaliana kwamba kuanzia tarehe Mosi julai mwaka huu baadhi ya maeneo ya Wapalestina ya Ukingo wa Magharibi (West Bank) yataunganishwa na ardhi iliyotwaliwa na utawala huo. Sambamba na hayo viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wamesema kuwa, iwapo Tel Aviv itatekeleza mpango huo hawataheshimu tena makubaliano yote ya usalama baina ya pande hizo mbili. Katika mkondo huo Abdullah Abdullah ambaye ni miongoni mwa makamanda wa harakati ya Fat'h amesema kuwa, ushirikiano uliokuwepo baina ya Mamlaka ya Ndani na utawala wa Kizayuni katika kupambana na virusi vya corona tayari umesimamishwa. 

Malalamiko ya Wapalestina ya kupinga mpango wa Israel wa kuyatwaa maeneo ya Ukingo wa Magharibi yanaongezeka siku baada ya nyingine. Israel inatumia malalamiko hayo kama kisingizio cha kuhalalisha ukandamizaji wake na vilevile kwa ajili ya kueneza propaganda chafu.

Kwa mfano tu Jumamosi ya jana wanajeshi wa Israel wamemuua kwa risasi kijana mmoja wa Palestina karibu na lango la Asbat katika mji wa Quds (Jerusalem) kwa kutumia kisingizio kwamba alikuwa amebeba kitu kinachofanana na silaha na kukificha kwenye nguo zake. Hata hivyo upekuzi uliofanyika baada ya mauaji hayo umebaini kuwa, kijana huyo wa Kipalestina hakuwa na silaha ya aina yoyote.

Wapalestina wanaendelea kuuawa shahidi kwa kipigwa risasi

Katika mauaji yaliyofanywa dhidi ya kijana wa Kipalestina huko Halamish pia askari wa Israel walidai kuwa, Mpalestina huyo alikuwa na nia ya kuwagonga kwa gari wavamizi wa Kizayuni.

Askari wa Israel pia wamevamia nyumba ya hatibu wa msikiti wa al Aqsa, Sheikh Ekrima Sa'id Sabri ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Palestina. 

Haya yote yanaonyesha kuwa, kushadidi kwa ukatili na machafuko baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel ni miongoni mwa matokeo ya mpango wa kibaguzi eti wa Muamala wa Karne na sera za kikoloni za utawala wa Kizayuni. Katika mazingira kama hayo pia kuna uwezekano mkubwa wa kushuhudiwa vita vipya au harakati mpya ya Intifadha baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni mwanzoni mwa mwezi wa Julai.    

Tags

Maoni