Jun 01, 2020 09:51 UTC
  • Israel yapanga kwa siri na Saudia namna ya kuwatwisha Wapalestina

Gazeti moja la utawala wa Kizayuni limeripoti kuwa, kumefanyika mazungumzo ya siri baina ya viongozi wa Israel na Saudi Arabia kuhusu kupewa Wasaudia usimamiaji wa maeneo matukufu ya mji wa Baytul Muqaddas kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne na kukabiliana na ushawishi wa Uturuki.

Gazeti la "Israel Hume" la utawala wa Kizayuni limeandika hayo leo Jumatatu na kuongeza kuwa, tangu mwezi Disemba 2019 viongozi wa Tel Aviv na Riyadh wamekuwa wakifanya mazungumzo ya siri kwa msaada na baraka kamili za Marekani. Viongozi wawili wa Saudi Arabia wamesema, kutokana na mikutano hiyo kuwa ya siri, ni wanadiplomasia na maafisa wachache sana wa usalama wa Israel, Marekani na Saudia ndio wenye taarifa na mazungumzo hayo.

Gazeti hilo la Kizayuni limeongeza kuwa, suala la kukabidhiwa Wasaudia jukumu la kusimamia na kuendesha maeneo matukufu ya Baytul Muqaddas limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu na kwa mujibu wa mipango mbalimbali ambayo imependekezwa hadi hivi sasa, Wajordan wataendelea kuwa wahusika wakuu wa kusimamia maeneo matakatifu katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds lakini maafisa wa Saudia watakuwa na jukumu la kusimamia kiutaalamu maeneo hayo.

Kibla cha Kwanza cha Waislamu kilipochomwa moto na Wazayuni

 

Gazeti hilo la Israel limeongeza kuwa, iwapo Wasaudia watakuwemo katika kusimamia maeneo matakatifu ya Palestina, jambo hilo litakuwa ni kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni na serikali ya Marekani na itakuwa rahisi kuwatwisha Wapalestina mpango wa "Muamala wa Karne"  uliopendekezwa na Marekani.

Mpango wa kidhulma wa "Muamala wa Karne" unasema kwamba mji wa Baytul Muqaddas wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa, ukabidhiwe kwa utawala wa Kizayuni, wakimbizi wa Palestina wapokonywe haki yao ya kurejea kwenye ardhi zao, na Wapalestina wapewe vijipande vidogo vidogo tu vilivyotapakaa hapa na pale katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza.

Tags

Maoni