Jun 01, 2020 09:53 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu hali mbaya ya uchumi wa Palestina wakati wa corona

Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu hatari ya matatizo ya kiuchumi na kuenea kirusi cha corona huko Palestina.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Nikolay Mladenov, mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Asia Magharibi akisema leo Jumatatu kuhusu matatizo ya kiuchumi ya Mamlaka ya Ndani ya Palesetina na Ukanda wa Ghaza kutokana na mzigo wa gharama za kukabiliana na maambukizi ya COVID-19 na kusisitiza kuwa, hatua za haraka zinahitajika kuzuia kutokea jambo hilo.

Vile vile amezungumzia matokeo mabaya yatakayotokea iwapo utawala wa Kizayuni utateka maeneo mengine ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuionya Israel isichukue hatua hiyo hatari.

Nikolay Mladenov

 

Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na serikali ya Donald Trump huko Marekani, umekusudia kupora asilimia 30 ya ardhi nyingine za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuziunganisha na ardhi nyingine za Palestina unazozikalia kwa mabavu kwa zaidi ya miongo 7 sasa.

Wakuu na makundi mbalimbali ya Palestina wanasema kuwa, hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa Marekani ulio dhidi ya Palestina uliopachikwa jina la "Muamala wa Karne" na ndio maana viongozi na makundi yote ya Palestina yakawa yanaunga mkono nia ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kuvunja ushirikiano wake na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tags

Maoni