Jul 02, 2020 06:42 UTC
  • Kuakhirisha kwa lazima Netanyahu mpango wa kutwaa ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan

Kuongezeka malalamiko na indhari hatimaye kumemlazimisha Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel aakhirishe mpango wake wa kutwaa ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuziunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina na sasa mpango huo utatekelezwa wakati mwingine.

Mwezi Aprili mwaka huu, Benjamin Netanyahu, kiongozi wa chama cha Likud na Benny Gantz kiongozi wa chama cha Blu na Nyeupe, walifikia makubaliano ya kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina. Mpango huo ulipangwa kuanza kutekelezwa jana tarehe Mosi Julai. Netanyahu alikuwa akikazania mno kutekelezwa mpango huo katika tarehe iliyokuwa imeafikiwa hapo kabla. Hata hivyo, mashinikizo yamemlazimisha asogeze mbele utekelezaji wake.

Utawala ghasibu wa Israel umekuwa ukikabiliwa na mashinikizo mengi kutoka kwa Wapalestina na hata katika uga wa kimataifa. Jana Jumatano Wapalestina walifanya maandamano makubwa dhidi ya Israel chini ya anuani ya ‘Siku ya Hasira’ maandamano ambayo yaliungwa mkono kimataifa. Jumuiya na asasi 16 za Palestina na za kimataifa zilitoa wito wa kufanyika maandamano hayo. Watumiaji wa mitandao ya kijamii nao walishiriki kwa kuweka jumbe mbalimbali kama #hapana-kutwaa, #hapana-kupora na kadhalika, na hivyo kuonyesha upinzani wao kwa mpango wa Israel wa kutaka kupora ardhi zaidi za Wapalestina.

Benjamin Netanyahu na Benny Gantz hasaimu wa kisiasa huko Israel

Fauka ya hayo, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukikabiliwa na indhari za makundi ya mapambano ya Palestina, indhari ambazo zinabeba ujumbe wa wazi wa uwezekano wa kutokea vita vipya endapo mpango huo wa kiharamia utatekelezwa. Katika uwanja huo, Abu Ubaida, Msemaji wa Brigedi za Ezzedin Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS, ametangaza kuwa makundi ya muqawama na ya kupigania ukombozi wa Paletina yataufanya utawala wa Kizayuni ujute kukalia kwa mabavu maeneo zaidi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Ameonya kuwa, kutekelezwa mpango huo kwa namna fulani kunatambuliwa kama ni kutangaza vita.

Nukta nyingine muhimu ni hii kwamba, Netanyahu amefahamu kuwa, bila himaya na uungaji mkono wa Marekani uwezekano wa kutekelezwa mpango huo unadhoofika au pasi na uungaji mkono wa Washington kiwango cha mafanikio ya mpango huo kitapungua. Kuanzia mwaka 2017 wakati Rais Donald Trump aliposhika hatamu za uongozi nchini Marekani hadi sasa, utawala haramu wa Israel umeendelea kutenda jinai nyingi dhidi ya Wapalestina kwa uungaji mkono wa serikali ya Washington hususan katika kufanya uporaji na uvamizi dhidi ya maeneo na ardhi za Wapalestina.

Vitongoji haramu vya walowezi wa Kiyahudi huko Palestina

Licha ya kuwa mpango wa kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina ni katika fremu ya mpango wa kibaguzi wa Marekani wa “Muamala wa Karne”, lakini inaonekana kuwa, kuna hitilafu kati ya White House na Tel-Aviv kuhusiana na wakati hasa wa kutekelezwa mpango huo. Kutokana na hali ya ndani inayoikabili Marekani kwa sasa, serikali ya Washington inaona kuwa huu si wakati bora na mwafaka wa kutekelezwa mpango huo.

Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana duru za habari zimetangaza kuwa, Netanyahu amesisitiza mbele ya wajumbe wa chama cha Likud kwamba, amekuwa na mazungumzo mazuri na chanya na viongozi wa Marekani, lakini mazungumzo hayo bado hayajafikia natija.

Jambo jingine ni kuwa, ili atekeleze mpango huo, Benjamin Netanyahu anahitajia uungaji mkono wa ndani pia ambapo hadi sasa mambo yamemuendea kombo kwani kuna upinzani dhidi ya mpango huo. Mbali na kuwa baadhi ya shakhsia na makundi ya Israel yanapinga utekelezwaji wa mpango wa kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina na hata kuonya kuhusiana na matokeo hasi ya hatua hiyo, ndani ya Baraza la Mawaziri pia kuna hitilafu kubwa za kimitazamo baina ya Benjamin Netanyahu na Beny Gantz, Waziri wa Vita na Gabi Ashkenazi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala dhalimu Israel.

Wanapambano wa Hamas

Gantz na Ashkenazi wanaamini kuwa, Netanyahu bado hajaondoka katika anga ya ushindani wa uchaguzi hivyo anataka kutumia utekelezwaji wa mpango huo hivi sasa kwa ajili ya kujinufaisha kisiasa.

Baadhi ya duru zimemnukuu Netanyahu akitangaza kuwa, Beny Gantz na chama chake cha Blu na Nyeupe hawatashiriki katika mazungumzo na Marekani kuhusiana na mpango wa kutwaa eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina. Kwa hakika anga jumla ya mazingira haya imekuwa sababu kuu ya Netanyahu kulazimika kuakhirisha kwa muda mpango wa kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina.

Maoni