Jul 03, 2020 09:46 UTC
  • Uturuki: Imarati imefanya jinai za kivita na mauaji ya kimbari huko Yemen

Mwakilishi wa kudumu Uturuki katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) imefanya jinai za kivita na mauaji ya kimbari katika vita vya Yemen.

Feridun Sinirlioğlu amemtumia ujumbe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akiashiria sera haribifu za Imarati nchini Yemen na uvamizi wake katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na kusema: Imarati ikishirikiana na Saudi Arabia na Marekani, ina nafasi kubwa katika kuwakandamiza watu wanaodhulumiwa wa Yemen na kuharibu miundombinu ya nchi hiyo.

Mwakilishi wa kudumu wa Uturuki katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, Imarati imetuma wapiganaji mamluki nchini Yemen, inayasaidia makundi ya kigaidi likiwemo la Daesh na inawalazimisha watoto kushiriki katika jinai hizo. 

Feridun Sinirlioğlu ameongeza kuwa, Imarati pia imefanya njama za kuipindua serikali ya Libya inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa kupitia njia ya kutuma n hini humo wapiganaji mamluki kutoka nchi za Sudan na Chad, lakini njama hiyo imefeli.

Maelfu ya watoto wa Yemen wameuawa katika mashambulizi ya Saudia na washirika wake.

Awali Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) lilikuwa limetangaza kuwa, Imarati inatuhumiwa kuwa imefanya jinai za kivita nchini Yemen kwa kutuma silaha za mabilioni ya dola kwa wapiganaji wa rais aliyejiuzulu na kukimbilia Saudi Arabia wa Yemen, Abdrabbuh Mansur Hadi. 

Mwezi Machi mwaka 2015 Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani, Imarati na Israel, ilianzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya taifa la Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa anga, baharini na nchi kavu. 

Maelfu ya Wayemeni wameuawa katika mashambulizi hayo na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo. 

Tags

Maoni